1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa Kuchunguza silaha za sumu Syria

28 Agosti 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema ataanzisha uchunguzi wa kimataifa juu ya matumizi ya silaha za sumu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka minne nchini Syria,

https://p.dw.com/p/1GNRC
Treffen zum Jemen in Genf
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Gillieron

Kauli hiyo imo kwenye barua ambayo Katibu Mkuu huyo aliliandikia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akielezea mipango yake ya kufanya uchunguzi kuhusu mashambuilizi hayo ya gesi ambao utaongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalokabiliana na silaha za sumu, OPCW.

Ban alisema lengo ni kutambua watu waliohusika katika vita hivyo kwa kiwango kikubwa, mashirika, makundi au serikali zilizochochea, kupanga, kufadhili au kuhusika katika matumizi ya kemikali za sumu ikiwemo Chlorine.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa uchunguzi huo utasimamiwa na msaidizi wake na manaibu wawili. Mapema kwenye taarifa yake Ban alisema kuwa matumizi ya silaha za kemikali za sumu katika mzozo wa Syria yanasikitisha.

Syrien Giftgasangriff Videostill September 2013
Wasyria wakifanya mazoezi ya jinsi ya kuwashughulikia waathiriwa wa silaha za sumuPicha: picture-alliance/AP Photo

Barua ya Ban inafuatia uamuzi ya tarehe 7 mwezi Agosti wa Baraza hilo la Usalama kukubali kufanyika uchunguzi. Baraza hilo linatarajiwa kumjibu Ban katika muda wa siku tano. Jopo hilo la uchunguzi litafanya kazi kwa mwaka mmoja lakini kipindi hicho kinaweza kuongezwa tena.

Serikali ya Syria na upinzani zimekana kutumia zana za sumu. Nayo mataifa ya Magharibi yanasema serikali ya Syria inahusika katika matumizi wa silaha za kemikali, ikiwemo matumizi ya Chlorine katika mashambulizi yake. Serikali za Syria na Urusi zimeshutumu waasi kwa matumizi ya gesi za sumu.

Ban alitakiwa kubuni jopo la uchunguzi baada ya Marekani kukubaliana na Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa Rais Bashar al-Asssad wa Syria kutaka kuanzishwa kwa uchunguzi.

Syria ilikubali kuharibu silaha zake za kemikali mwaka 2013 ili kuepuka mashambulizi kutoa vikosi vya jeshi la Marekani baada ya kutuhumiwa kutumia gesi za sumu na kuuwa mamia ya raia. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Silaha za Sumu limethibitisha kuwa kuna matumizi ya chlorine ya mara kwa mara lakini bado halijatambua muhusika hasa.

Uchunguzi mwingine uliofanywa na Shirika la Umoja Wa Mataifa ulibaini kuwa gesi ya sarin pia ilikuwa imetumika kuua nchini Syria lakini uchunguzi huwo ukajizuia kutoa lawama kwa kundi lolote.

Matumizi ya chlorine yamekatazwa chini ya mkataba wa kimataifa kuhusu matumizi ya silaha za kemikali, mkataba ambao Syria ilijiunga nao 2013.

Den Haag OPCW Zentrale LOGO
Makao makuu ya shirika la umoja wa mataifa la kukabiliana na matumizi ya silaha za sumu OPCWPicha: picture-alliance/epa/Daniels

Ikiwa mtu anavuta gesi ya chlorine, gesi hiyo inabadilika na kuwa tindikali ya hydrochroric kwenye maini, ambayo ni hatari kwa uhai wa binaadamu.

Mapema juma hili, Shirika la Madaktari Wasio Mipaka, MSF, lilisema kuwa limewahudumia raia walioathiriwa na aina fulani ya kemikali huko Marea, mji ulio karibu na jiji la Aleppo, kufuatia mashambulizi ya wiki iliyopita. Chama cha Madaktari wa Syria na Marekani, SAMS, waligundua gesi hiyo kuwa gesi hatari.

Wakati huo huo, afisa wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo ulishindwa kuwasilisha misaada ya kibinadamu kwa raia elfu 422 mnamo mwezi wa Julai katika maeneo yaliyokumbwa na vita huku hali ikiendelea kuwa mbaya.

Afisa huyo wa maswala ya kibinadamu, Stephen O'Brien alisema watu wanaendelea kuteseka katika hali hiyo ya vita huku akiongeza kuwa watu wengine milioni 4.6 wanaishi katika maeneo ambayo hayawezi kufikiwa. Ni asilimia 12 pekee kati yao ndio ambao wamepokea msaada wa chakula katika miezi michache iliyopita.

Mwandishi: Bernard Maranga/Reuters/AFP/DPA

Muhariri: Mohammed Khelef