1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kumuunga mkono Hadi

23 Machi 2015

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kumuunga mkono Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi. Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa Yemen, ameonya nchi hiyo itatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/1EvPJ
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Katika kikao chake cha dharura mjini New York hapo jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pia lilielezea dhamira yake kubwa ya kuunga mkono suala la kuwepo umoja, uhuru na mshikamano wa Yemen, na nia yake thabiti ya kusimama pamoja na watu wa nchi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na wanachama 15 wa baraza hilo na wamefafanua kwamba wanaunga mkono uhalali wa Rais Hadi na wametishia kuweka vikwazo zaidi dhidi ya wanamgambo wa Kishia wanaojulikana kama Houthi, ambao wanaudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Sanaa.

Kikao cha baraza hilo kimefanyika wakati ambapo Yemen inakumbwa na mashambulizi, yakiwemo yale ya kujitoa muhanga wiki iliyopita katika misikiti mjini Sanaa na kuwaua watu 142. Kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu-IS limekiri kuhusika na mashambulizi hayo.

Rais wa Yemen, Abed Rabbo Mansour Hadi
Rais wa Yemen, Abed Rabbo Mansour HadiPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo//H.Mohammed

Uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, umefikiwa baada ya Rais Hadi kuliomba baraza hilo kupitia barua kufanya kila liwezekanalo kuingilia kati haraka. Akizungumza katika mji wa kusini wa Aden, ambao ameutangaza kuwa mji mkuu wa muda, Rais Hadi amewataka waasi wa Houthi, kuondoka kwenye mji mkuu, Sanaa pamoja na miji mingine.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Yemen, Jamal Benomar
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Yemen, Jamal BenomarPicha: UN Photo/Rick Bajornas

Ama kwa upande mwingine, Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamal Benomar ameonya kuwa nchi hiyo inaelekea kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Akizungumza na baraza hilo kwa njia ya video kutoka Doha, Qatar, Benomar amesema ghasia za Yemen zinafanana na mizozo ya Iraq, Libya na Syria.

Hadi amlaumu mtangulizi wake

''Matukio ya wiki na siku za hivi karibuni yanaonekana kuitoa Yemen katika amani na kuipeleka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tangu Rais Hadi awasili Aden, ameanzisha kile kinachoitwa kamati inayomtii, ambayo sasa inaidhibiti Aden na anamtuhumu kiongozi wa zamani, Rais Ali Abdullah Saleh na waasi wa Houthi kwa kufanya mapinduzi dhidi yake,'' alisema Benomar.

Benomar amezitaka pande zinazohasimiana kujizuia na mapigano na kuacha kutumia nguvu na amesema ili nchi hiyo iweze kusonga mbele, amani itapatikana kwa njia ya mazungumzo pekee.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power amesema watu wa Yemen wanazidi kujikuta katika hali mbaya, kwani wataendelea kukumbwa na madhara iwapo pande zote hazitoacha mapigano mara moja na kuirejesha Yemen katika kipindi cha mpito cha kisiasa.

Waasi wa Houthi
Waasi wa HouthiPicha: REUTERS/K. Abdullah

Wakati huo huo, waasi wa Houthi wametangaza upya hatua yao ya kuitwaa miji yote ya Yemen, kutokana na mashambulizi ya wiki iliyopita. Hapo jana, waasi hao waliuteka mji wa Taiz, ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini Yemen.

Kiongozi wa waasi, Abdulmalik al-Huthi amewasihi Wayemen kuhamasishana na kujiunga na wapiganaji wake dhidi ya Dola la Kiislamu na Al-Qaeda kusini mwa nchi hiyo. Huthi pia ametishia kujiondoa katika mazungumzo kati ya makundi pinzani ya Yemen, yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, akikataa pendekezo la Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Josephat Charo