1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kutuma waangalizi Syria

15 Aprili 2012

Kundi la kwanza la waangalizi wa Umoja wa Mataifa linawasili nchini Syria Jumapili, kusimamia usitishwaji wa mapigano, wakati kuongezeka kwa ghasia nchini humo kukitishia juhudi za kusimamisha umwagaji damu.

https://p.dw.com/p/14e8t
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laidhinisha waangalizi Syria
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laidhinisha waangalizi SyriaPicha: Reuters

Urusi na China zimeunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kupelekwa kwa waangalizi hao, hii ikiwa mara ya kwanza kwa wanachama wote 15 wa baraza hilo kukubaliana juu ya Syria tangu kuanza kwa mgogoro nchini humo miezi 13 iliyopita.

Msemaji wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nchini Syria, Kofi Annan alisema Jumamosi kuwa waangalizi sita wa kwanza wangewasili nchini Syria katika muda wa saa 24 na kuanza kufanya kazi katika muda wa saa 36. Kwa mujibu wa msemaji huyo, waangalizi wengine watawasili siku zinazofuata.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameiambia redio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, kuwa atahakikisha kundi la awali la waangalizi linatumwa haraka iwezekanavyo, na kwamba ifikapo tarehe 18 April litakuwa limewasilisha mapendekezo juu ya ujumbe rasmi wa waangalizi.

Ghasia zaendelea

Wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipokuwa likipiga kura, nchini Syria ghasia zilikuwa zikipamba moto. Wanaharakati wamesema kuwa kwa uchache watu sita waliuawa katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Mtaa wa Homs ambao wapinzani wamesema umeendelea kushambuliwa na jeshi la serikali
Mtaa wa mji wa Homs ambao wapinzani wamesema umeendelea kushambuliwa na jeshi la serikaliPicha: Reuters

Kulingana na ripoti ya wanaharakati hao, vikosi vitiifu kwa Rais Bashar al Assad viliushambulia kwa mabomu mji wa Homs ambao ni ngome ya upinzani, hayo yakiwa mashambulizi ya kwanza tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa amani wa Kofi Annan siku tatu zilizopita.

Picha za video ambazo mpigaji wake alisema ni kutoka kitongoji cha al-Qarabis katika mji wa Homs zimeonyesha vifaru viwili vikipita kwa kasi mitaani, huku miripuko na milio ya risasi vikisikika. Serikali ya Syria imekuwa ikiwalaumu ''magaidi'' kwa njama za kumpindua Rais Bashar al Assad. Shirika la habari la serikali SANA limesema kuwa ''magaidi wenye silaha'' wamewaua watu watano na kumteka nyara mbunge kutoka eneo la kaskazini. Jeshi pia lilisema kuwa afisa wa cheo cha Kanali alichukuliwa mateka katika mjo wa Hama. Ni vigumu kuhakikisha ukweli ripoti zinazotolewa kwa sababu waandishi wa habari wamezuiliwa.

Jukumu kubwa ni la serikali

Ban  Ki-moon amesema serikali ndio yenye jukumu kubwa la kusimamisha ghasia na kuondoa vikosi vyake kutoka mijini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema serikali ya Syria inapaswa kuwajibika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema serikali ya Syria inapaswa kuwajibikaPicha: Reuters

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani ''ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na serikali, na uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na makundi yenye silaha''.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa jeshi Syria limeuwa watu 9,000 tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga utawala wa rais Assad. Serikali inasema wanamgambo wanaoungwa mkono na nchi za kigeni wameuwa maafisa wa usalama 2500.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE

Mhariri: Stumai George