1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuwawekea vikwazo viongozi wa M23

29 Novemba 2012

Licha ya waasi wa M23 kutangaza kujiondoa kwenye mji wa Goma, Umoja wa Mataifa unasema waasi hao hawajaonesha dalili ya kuondoka kabisa na umetoa wito kwa mataifa ye kigeni kutojihusisha na mgogoro kwenye eneo hilo.

https://p.dw.com/p/16sMD
Mkuu wa tawi la kisiasa la M23, Jean Marie Runiga.
Mkuu wa tawi la kisiasa la M23, Jean Marie Runiga.Picha: Junior D. Kannah/AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa kundi la waasi wa M23 na vile vile watu wanaowaunga mkono kutoka nje. Kwenye azimio lililopitishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama, Umoja huo umewataka waasi wa M23 kuweka silaha zao chini na kuacha mapigano mara moja na pia kuwaachilia watoto wanaohudumu kwenye kundi lao kama wapiganaji.

Likionesha wasiwasi wake kufuatia taarifa za mauaji, ubakaji na kuajiriwa watoto kwenye kundi la M23, Baraza la Usalama limeelezea nia ya ya kuwawekea vikwazo viongozi wa kundi hilo na watu wanaoaminika kuliunga mkono. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni kupiga marufuku ya uuzwaji wa silaha kwa makundi ya waasi wa Kongo.

Serikali ya Kongo ndiyo yenye jukumu la kulinda watu wake

Vile vile Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Rais Joseph Kabila kuendesha uchunguzi na kuwaadhibu waliohusika na uhalifu huo, kwani "usalama na amani ya Kongo ni jukumu la kwanza la serikali hiyo."

Marais Yoweri Museveni wa Uganda (kushoto), Joseph Kabila wa DRC (katikati) na Paul Kagame wa Rwanda katika mkutano wa viongozi wa Maziwa Makuu juu ya mzozo wa Kivu ya Kaskazini, Novemba 2012.
Marais Yoweri Museveni wa Uganda (kushoto), Joseph Kabila wa DRC (katikati) na Paul Kagame wa Rwanda katika mkutano wa viongozi wa Maziwa Makuu juu ya mzozo wa Kivu ya Kaskazini, Novemba 2012.Picha: dapd

Msimamo huo unafuatia lawama dhidi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO) ambacho hakikuzuwia kutekwa kwa mji wa Goma na waasi wa M23 wiki mbili iliopita.

Baraza hilo limeyatahadharisha makundi yote ya wapiganaji katika mashambulizi yao dhidi ya walinda amani wa MONUSCO na raia wa kawaida. Baadaye, Baraza la Usalama lilipitisha azimio linaloidhinisha ripoti ya wataalamu kuhusu Kongo.

Mataifa ya kigeni yalaumiwa

Akizungumza na DW mjini New York, Naibu Balozi  wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Olivier Nduhungirehe, alisema nchi yake inakubaliana na hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa, lakini aliendelea kukanusha kuhusika kwa nchi yake na mzozo wa Kongo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekanbi, Hillary Rodham Clinton.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekanbi, Hillary Rodham Clinton.Picha: dapd

"Rwanda siyo chanzo cha mzozo wa Kongo na haijihusishi hata kidogo. Tumeshangazwa sana na msimamo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono ripoti ya kundi la wataalamu inayoelezea kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23, bila ya Baraza hili kuhoji mfumo wa uchunguzi, ushahidi na tuhuma za wataalamu hao dhidi ya Rwanda." Alisema Balozi Nduhungirehe.

Balozi wa Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo nchini Ufaransa, Ileka Atoki, alielezea msimamo wa nchi yake kwamba inataka viongozi wa Rwanda waliotajwa kwenye ripoti hiyo wawekewe vikwazo.

"Ushahidi wa watu na vifaa umetambuliwa na Umoja wa Mataifa kuthibitisha kuvamiwa kwa Kongo na nchi ya Rwanda. Mbali na hayo, Rwanda inaendelea kukiuka marufuku ya Umoja wa Mataifa ya kutowapa silaha wapiganaji na kusababisha hali mbaya ya kiutu kwenye mkoa wa Kivu ya kaskazini. Kutokana na mauwaji hayo, serikali ya Kongo na jumla ya raia wake wote wanasubiri kuona hatua kali zikichukuliwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya wahusika wa machafuko hayo."

Baada ya azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kiongozi wa Kamati ya Vikwazo vya Umoja huo anatarajiwa kuwasilisha orodha ya majina ya watu watakaowekewa vikwazo mwishoni mwa wiki hii.

Duru za kuaminika za Umoja wa Mataifa zimeimbia DW kwamba Umoja huo utafuatilia kwa karibu kutekelezwa kwa matokeo ya Mkutano wa Marais wa Nchi za Maziwa Makuu kuhusu usitishwaji mapigano na kuondoka kwa waasi kwenye mji wa Goma.

Mataifa ya Magharibi yaendelea na diplomasia

Hatua hii inakuja katika wakati ambapo Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaendesha juhudi maalumu za kidiplomasia katika mataifa ya Kongo, Rwanda na Uganda ili papatikane suluhisho la mzozo wa hivi sasa kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

Waasi wa M23 wakipiga doria kwenye mji wa Goma.
Waasi wa M23 wakipiga doria kwenye mji wa Goma.Picha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amewatolea wito viongozi wote wa eneo la Maziwa Makuu kusitisha kuwasaidia waasi wa M23.

Akigusia ukweli kwamba kiasi cha watu 285,000 wameshayakimbia makaazi yao tangu waasi hao waanze kuelekea mjini Goma mwezi Aprili, Clinton amesema wengi wa watu hao wanahitaji msaada wa dharura na akawataka waasi kuacha mashambulizi na kujiondoa moja kwa moja mjini Goma.

"Tunawatolea wito viongozi na serikali zao katika eneo zima kusita na kuzuia msaada wowote kwa M23 kutoka ndani ya mipaka za nchi zao." Alisema Clinton katika kile kinachotajwa kuwa ni kauli nzito zaidi kuitoa tangu mzozo huu kulikumba eneo la Maziwa Makuu.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW New York
Mhariri: Mohammed Khelef