1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa na Malengo ya Melinia

Othman,Miraji10 Septemba 2008

Malengo ya Melinia yadurusiwa mjini Berlin

https://p.dw.com/p/FFW4
Waziriwa Ujerumani wa Ushirikiano wa Kiuchumi, Bibi Heidemarie Wieczorek-ZeulPicha: AP

Lengo lilowekwa na Umoja wa Mataifa ni kwamba ifikapo mwaka 2015 umaskini duniani upunguke kwa nusu. Mwishoni mwa mwezi wa Novemba na mwanzoni mwa Disemba mwaka huu kutafanywa mkutano wa kimataifa mjini Doha, Qatar, kuangalia kimefikiwa nini hadi sasa. Na kuutayarisha mkutano huo, jana walikutana mjini Berlin, hapa Ujerumani, mabingwa kutoka nchi kadhaa fadhili na zile zinazopokea misaada na wakazungumzia vipi malengo ya Milenia juu maendeleo yanavogharimiwa, kifedha.

Pale waziri wa Ujerumani wa Ushirikiano wa Kiuchumi, Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul, alipowajulisha watu miezi miwili iliopita ripoti juu ya siasa ya maendeleo ya Ujerumani, alizitaja tarakimu zinazotisha. Lakini licha ya hayo, waziri huyo wa misaada ya maendeleo alifurahishwa na mambo fulani. Alisema kwa mara ya kwanza idadi ya watu maskini walio hohe hahe duniani, watu wanaolazimika kuishi kwa chini ya dola moja ya Kimarekani kwa siku, imepunguwa na kufikia chini ya watu bilioni moja. Mwaka 1990 idadi ya watu wa aina hiyo ilifikia bilioni 1.25. Pia katika kipindi hicho hadi sasa, idadi ya wakaazi wa dunia imeongezeka kutoka bilioni 5.3 na kuwa bilioni 6.7.


Hata hivyo, jamii ya kimataifa iko mbali kulifikia lile lengo la kupunguza kwa nusu idadi ya walio maskini duniani, ifikapo mwaka 2015. Ndio maana waziri huyo wa Ujerumani akazungumzia juu ya sura ya mchanganyiko ilioko sasa ambapo nusu ya kipindi kilichowekwa imefikia. Maendeleo yamefanyika katika sekta za elimu, afya na kusamehe madeni. Idadi ya watoto wanaokwenda shule huko Ghana, Tanzania, Uganda na Msumbiji imeweza kuongezeka sana na watu milioni mbili walio na ugonjwa wa AIDS wameweza kuhudumiwa kila wakati: Hayo ni mafanikio, alisema Bibi Wieczorek-Zeul, lakini pia ni changamoto la kufanya mengi zaidi:


" Dunia inatumia dola bilioni 1,300 kwa ajili ya silaha na dola bilioni 103, yaani moja kwa kumi, kwa ajili ya ushirikiano na ujenzi wa kiuchumi. Ni lazima tubadilishe namna wapi tunatilia mkazo, ili dunia iweze kuwa mahala pa maisha ya amani na yasiokuwa na utumiaji nguvu."


Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul inabidi awe na uhakika wa kuungwa mkono na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon. Yeye ni mwakilishi wake maalum katika mkutano juu ya kugharimia maendeleo utakaofanyika huko Doha. Wadhifa huo huo anao pia waziri wa fedha wa Afrika Kusini, Trevor Andrew Manuel, ambaye naye anapigania zitolewe fedha zaidi na kuweko uwazi katika ushirikiano wa kiuchumi. Huo ni mwito ulioelekezwa kwa nchi fadhili na zile zinazopokea misaada.


Karibu miaka minane iliopita, pale malengo ya Mellenium yalipotangazwa hakujakuweko tatizo la kupanda juu sana bei za vyakula, hali ambayo imewabana zaidi watu walio maskini katika Afrika na Asia. Na kwa mujibu wa waziri huyo wa fedha wa Afrika Kusini, suluhisho liko katika kuweko biashara huru duniani:


+ Yaonesha sababu ya kuweko matatizo katika kilimo ni kushindwa yale mashauriano ndani ya Shirika la Biashara Duniani. Hakuna motisha hata kidogo wa kukuza kilimo. Katika Afrika kuna ardhi nyingi ilio na rutuba, lakini kuna upungufu wa miundo mbinu kuweza kuitumia uzuri ardhi hiyo."


Mawaziri Trevor Manuel na Heidemarie Wieczorek-Zeul wanakubaliana kwamba Uchina inaweza ikatoa mchango mkubwa katika kupambana na umaskini duniani. Tatizo , alisema waziri wa Kijerumani, ni kwamba Uchina bado inajiona kuwa ni nchi ya kupokea misaada. Wakati huo huo, Uchina inajitokeza kama nchi fadhili, hasa huko Afrika, harakati ambazo Bibi Wieczore-Zeul anazitilia wasiwasi.


Nchi za Magharibi zinailaumu Uchina kwamba inajaribu kutumia misaada ya maendeleo ili kujihakikishia kuwa na masoko ya mali ghafi, hasa barani Afrika.