1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama akutana na Putin New York

28 Septemba 2015

Mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na,hotuba ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck kuhusu wakimbizi ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini

https://p.dw.com/p/1GeaE
Kansela Angela Merkel(kushoto),katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon wakizungumza pembezon i mwa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/S. Kugler

Tuanzie lakini New York unakoendelea mkutano wa 70 wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa.Mhariri wa gazeti linalosomwa na wengi la "Bild" anaandika:" Katika kikao hiki cha sasa lazma itolewe ishara!Maneno matupu basi tena-matatizo ya ulimwengu yanahitaji kushughulikiwa kivitendo.Wakaazi wa Syria na Afrika hawaondoki kwa kutaka!Wanakimbia vita,kuandamwa,na shida za maisha.Hawahitaji maneno matupu,wanataka kuona vitendo!Ndio maana mipango ya madola makuu,kutokomesha umaskini na njaa ulimwenguni na kuruhusu uhuru wa mtu kutoa maoni yake,itakuwa na maana tuu ikiwa itatekelezwa mara moja.Na kama hapatafikiwa maridhiano pamoja na waimla na makatili mfano wa Assad wa Syria.Umoja wa Mataifa unabidi ugeuke taasisi yenye nguvu.Taasisi inayosubutu kuyataja maovu kuwa ni maovu na kuchukua hatua zinazostahiki.La sivyo matokeo ya mkutano wa hadhara kuu mjini New York yatakuwa kwa mara nyengine tena,hayana maana yoyote-yatasalia karatasini tu.

Baraack Obama kukutana na Vladimir Putin

Mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa unatoa fursa ya kukutana upya na baada ya kupita muda mrefu marais Barack Obama wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi.Gazeti la "Märkische Allgemeine" linaandika:"Itakuwa sawa na kutia chunvi tukitaraji makubwa katika mkutano wa leo kati ya Barack Obama na Vladimir Putin,hata kama ni mazungumzo yao ya kwanza baada ya muda mrefu.Hata hivyo kuna kila sababu ya kujiwekea matumaini,kutaraji kuna kitakachotokea,ili kuwapunguzia machungu wananchi wa Syria.Kwasababu mazungumzo kati ya Obama na Putin na duru nyengine kadhaa za mazungumzo yatakayofanyika mnamo siku zinazokuja katika vyumba na kumbi za makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York ,yanasadifu wakati ambao,wamarekani,warusi,wazungu wa Ulaya,wairan na waarabu wanajikuta wakishinikizwa wapitishe maamuzi.Kuna sababu mbili:kwanza:mzozo wa wakimbizi unaozifanya nchi za Ulaya ziyaone moja kwa moja madhara ya vita, na pili: vifaru vya Urusi kwa Syria na ushirikiano kati ya Urusi na Iran katika ardhi ya Irak wenye lengo la kuwashinda nguvu ISIL,ni kitisho kwa wamarekani na waarabu.

Hotuba safi ya rais Gauck kuhusu wakimbizi

Mzozo wa wakimbizi ndio kiini cha hotuba ya rais wa shirikisho Joachim Gauch alipokuwa anafungua "wiki ya kanisa ya ushirikiano wa tamaduni" mjini Mainz jana usiku.Gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" linaandika:"Rais wa shirikisho Joachim Gauck amesifu mshikamano wa wajerumani na kuchambua kwa kina changamoto zinazoikabili nchi hii.Hakuficha chochote alipozungumzia mahitaji ya wakimbizi.Amewakaribisha wawe sehemu ya jamii ya nchi hii ikiwa watakuwa tayari kuheshimu,sheria,uhuru,haki za binaadam na haki sawa za kijinsia.Matamshi yake yanaweza kutuliza wahka wa wiki zilizopita na kuchangia kuanzisha mjadala wa maana.Kwa sababu alichokisema kinaweza kukubaliwa na wote: tangu wale ambao daima wamekuwa wakiishi nchini Ujerumani mpaka kufikia wale wanaoingia humu nchini kama wakimbizi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman