1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa umemkosoa rais wa Venezuela

Mohammed Abdulrahman
30 Juni 2017

Umoja wa Mataifa leo umeikosoa serikali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kwa kupunguza madaraka ya mwendesha mashtaka mkuu na kuitaka iheshimu utawala wa kisheria pamoja na haki ya watu kukusanyika.

https://p.dw.com/p/2fiJM
Venezuela Caracas Anti Maduro Protest
Waandamanaji wanaompinga Rais Nicolaus Maduro wa VenezuelaPicha: Reuters/I. Alvaro

Wito huo wa Umoja wa mataifa umetolewa  wakati serikali  ya Maduro ikiendelea kukandamiza maandamano ya upinzani. Wapinzani wa Maduro wanamiminika  mabarabarani takriban kila siku kwa miezi mitatu sasa, kupinga kile wanachokiita  kuundwa kwa utawala wa kidikteta. Maandamano hayo yaliosababisha hadi sasa karibu watu 80 kuuwawa, mara nyingi huishia kwenye machafuko na mapambano na  askari wa usalama.

Maafisa wa chama tawala cha Kisoshalisti, wametoa mloongo wa matamshi ya kumshambulia mwendesha mashtaka mkuu Luisa Ortega ambaye amekuwa akihudumu pia kama Mwanasheria mkuu,  kwamba anachochea  machafuko baada ya kujitenga na msimamo wa serikali.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa ya Geneva

Schweiz Rupert Colville
Msemaji wa Umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya Haki za Binaadamu Rupert ColvillePicha: AFP/Getty Images

Msemaji wa  Umoja wa mataifa anayehusika  na  masuala ya Haki za Binaadamu Rupert Colville, alitoa taarifa mjini Geneva akisema, uamuzi wa mahakama ya Venezuela tarehe 28 mwezi huu wa Juni kuanza  mchakato wa muondoa katika wadhifa wake mwanasheria mkuu, kuzizuwia mali zake na kumzuwian pia kusafiri nje ya nchi, ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa sawa na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Colville alisema mahakama kuu ya katiba kwa upande mwengine imefuta uteuzi wa Bibi Ortega wa  naibu mwanasheria mkuu na kumteuwa mtu mwengine, ikiwa ni kinyume cha sheria.Pia Bibi Ortega amepokonywa baadhi ya majukumu yake na kupewa mtu mwengine.

Tangu mwezi Machi, Mwanasheria mkuu huyo amechukua hatua muhimu kulinda haki za binaadamu, akisisitiza  juu ya  kutengwa kwa madaraka na maamuzi kulingana na sheria na kuwataka watu waliokamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria waachiliwe huru.

Rais Maduro anadai kwamba maanadamno ya wapinzani yanayolenga katika  kuiangusha serikali yake kwa msaada wa Marekani.

Kwa upande mwengine Umoja wa mataifa umesema umepokea taarifa kwamba askari wa usalama wameyavamia majengo kadhaa ya makaazi, kufanya upekuzi bila ya kibali , kuwaandama  wafuasi wa upinzani na kuwakamata watu hovyo. Inasemekana lengo hasa ni kuwazuwia watu wasishiriki katika maandamano ya kuipinga serikali.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman Reuters
Mhariri: Iddi ssesanga