1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waambiwa mauaji yanaendelea nchini Syria

Mohammed Khelef11 Januari 2012

Umoja wa Mataifa umesema kwamba kiasi ya watu 400 wameuawa nchini Syria tangu timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Kiarabu ianze kazi ya kuangalia utekelezaji wa mpango wa amani mwezi Disemba mwaka jana.

https://p.dw.com/p/13hKz
Waombolezaji wakiswalia maiti mjini Damascus.
Waombolezaji wakiswalia maiti mjini Damascus.Picha: Reuters

Vyanzo vya kibalozi vinasema kwamba Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya siasa, Lynn Pascoe, ametoa takwimu hiyo katika mkutano wa ndani wa Baraza la Usalama. Umoja wa Mataifa unakisia kuwa zaidi ya watu 5,000 wameshauwa, tangu maandamano ya kupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad yaanze mwezi Machi mwaka jana.

Wakati huo huo, timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Kiarabu imevamiwa na wafuasi wa Assad na magari yao kuharibiwa. Kituo cha Al Jazeera kimeonesha picha za magari hayo na kumhoji mmoja wa waangalizi aliyejiuzulu kutokana na kile alichokiita "upotoshaji wa serikali."

Hapo jana Rais Assad alilihutubia taifa na kuapa kwamba angelipambana na magaidi kwa nguvu zote. Pia aliilaumu jumuiya ya kimataifa kwa kuihujumu nchi yake na Jumuiya ya Kiarabu kwa kushindwa kulinda maslahi ya Waarabu.

Vurugu ziliendelea hapo jana ambapo kundi la haki za binaadamu la Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza limesema watu 10 waliuawa na wengine 40 kujeruhiwa katika mji wa mashariki wa Deir Ezzor pale vikosi vya serikali vilipowashambulia waandamanaji. Ripoti kutoka nje ya Syria ni shida kuthibitishika kutokana na serikali kupiga marufuku waandishi wa habari wa kigeni.