1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa wakasirishwa na mauaji ya wanajeshi wa UNAMID

10 Julai 2008

Wanamgambo wa Janjaweed washukiwa kuhusika

https://p.dw.com/p/EZXT
"Wanajeshi sabaa wa UNAMID waliuwawa "Picha: AP

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mauaji ya wanajeshi sabaa wa jeshi la pamoja la Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika la kuweka amani katika jimbo la mzozo la Darfur nchini Sudan.

Msemaji wa katibu mkuu Michelle Montas amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba katibu mkuu Ban Ki Moon anaitaka aserikali ya Sudan kuwasaka na kufikisha mbele ya sheria wahusika wote wa kitendo hicho ambacho hakikubaliki hata kidogo.

Katika shambulio hilo ambalo linashukiwa kufanywa na wanamgambo wa Janjaweed wanajeshi wengine 22 walijeruhiwa sabaa kati yao vibaya sana.

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa wanajeshi hao walipigana kwa muda wa saa mbili na wanamgambo waliokuwa na silaha nzito nzito ikiwemo roketi.

Magari kumi ya kikosi hicho cha Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika cha UNAMID yaliharibiwa vibaya.

Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa pia umelaani shambulio hilo ambalo umelitaja kuwa la kihalifu.