1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatafuta dola bilioni 4.2 za kuisaida Ukraine mnamo 2024

Zainab Aziz
15 Januari 2024

Umoja wa Mataifa umesema unahitaji dola bilioni 4.2 mwaka huu ili kuuwezesha kutoa msaada kwa mamilioni ya watu waliokimbia vita kutoka nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4bGBi
UN-Sicherheitsrat tagt zur Ukraine | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Spencer Platt/Getty Images/AFP

Umoja wa Mataifa umewatolea mwito wafadhili wachange dola hizo bilioni 4.2 kwa ajili ya kuzisaidia jamii nchini Ukraine zinazokabiliwa na vita na mgogoro wa wakimbizi wa Ukraine huku vita vikiendelea kupamba moto karibu miaka miwili tangu nchi hiyo ilipovamiwa na  Urusi.UN: Watu wapatao milioni 8 wamekimbia kutoka Ukraine tangu uvamizi wa Urusi

Mkuu katika Umoja wa Mataifa anayesimamia maswala ya misaada Martin Griffiths amesema katika miji midogo na vijiji vilivyo kwenye mstari wa mbele wa vita, watu wamemaliza rasilimali zao zote na sasa wanategemea misaada inayoingizwa na misafara ya washirika wa Umoja wa Mataifa ili kujikimu maisha.

Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuchanga mabilioni ya dola kwa ajili ya Ukraine l Martin Griffiths
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura (OCHA), Martin Griffiths wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa pamoja wa mpango wa kukabiliana na wakimbizi wa Ukraine.Picha: Martial Trezzini/dpa/Keystone/picture alliance

Griffiths amesema katika mikoa ya Donetsk na Kharkiv, familia zinaishi katika nyumba zilizoharibiwa na hakuna maji ya bomba, gesi au umeme. Amesema familia hizo zinakabiliwa na hali ngumu hasa katika msimu huu wa baridi kali.

Ukraine inasonga mbele na mpango wake wa amani kwa lengo la kuvimaliza vita na Urusi.  Mpango huo ulijadiliwa kwenye mkutano wa maafisa wa usalama wa taifa, kutoka duniani kote katika mji wa Davos. Kikao hicho kiliwaleta pamoja washiriki zaidi ya 80 kutoka nchi na mashirika ya kimataifa.

Soma Pia:Zelensky kuizuru Uswisi kuimarisha uungaji mkono wa kimataifa

Mwakilishi wa rais Zelensky, Andriy Yermak amesema inahitajika kuishirikisha China katika mazungumzo ya kumaliza vita na Urusi, baada ya kumalizika mkutano wa ngazi ya juu wa kidiplomasia kuhusu Ukraine uliofanyika kabla ya Kongamano la Kiuchumi la Dunia la Davos nchini Uswisi.

Uswisi, Davos | Kongamano la Kiuchumi Duniani
Davos, Uswisi | Kongamano la Kiuchumi Duniani - Nembo ya Kongamano la Kiuchumi Duniani ikionyesha kwenye dirisha katika Kituo cha Mkutano huko Davos, Uswisi, Jumapili, Januari 14, 2024. Mkutano wa kila mwaka wa Kongamano la Kiuchumi Duniani unafanyika Davos kuanzia Januari 15 hadi Januari .19,Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Yermak amesema ni muhimu kwamba mshirika wa Urusi, China ilikuwepo kwenye mkutano wa Jumapili na wakati ambapo Ukraine inapanga kuitisha mikutano zaidi juu ya kanuni yake kuelekea amani.

Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy anatarajiwa aliwasili mjini Bern, Uswizi Jumatat 15.01.2024 ambako atakutana na Rais wa Uswisi Viola Amherd.Zelenyk atahudhuria Kongamano la Kiuchumi la Dunia linaloanza Jumanne 15.01.2024 hadi 19.01.2024.

Uswisi  l  Davos  l  Volodymyr Zelensky
Mbele: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky baada ya kuwasili nchini Uswisi nyuma yake mwenye vazi jekundu ni waziri wa mambo ya nje wa Uswisi diwani Ignazio Cassis. Picha: Alessandro Della Valle/dpa/picture alliance

Taarifa kutoka ikulu ya Urusi imesema mazungumzo ya Davos juu ya mapendekezo ya amani yaliyowasilishwa na Ukraine  hayatafanikiwa kutokana na kwamba Urusi haikushiriki katika majadiliano.

Soma Pia:Rais Zelensky atarajia msaada zaidi wa ulinzi wa anga

Urusi imesisitiza kwamba itaendelea na operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine hadi itakapofikia malengo yake yote.

Vyanzo:RTRE/AFP