1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waongeza wanajeshi Cote d'Ivoire

20 Januari 2011

Baada ya mjumbe wa Umoja wa Afrika, kukiri kushindwa kumshawishi Laurent Gbagbo kuondoka madarakani, Umoja wa Mataifa watangaza kuongeza idadi ya wanajeshi katika kikosi chake cha kulinda amani nchini Cote d'Ivoire.

https://p.dw.com/p/zzxx
Kikosi cha UNOCI kikilinda mjini Abdijan
Kikosi cha UNOCI kikilinda mjini AbdijanPicha: picture alliance/landov

Mjini New York, Marekani, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la umoja huo, limeagiza kwamba wanajeshi 2,000 waongezwe katika kikosi chake cha UNOCI nchini Cote d'Ivoire. Hii ni kufuatia taarifa za makamanda wake walioko mjini Abdijan, ambao wanahofia mapigano kati yao na vikosi vitiifu kwa Laurent Gbagbo, ambavyo vinayazingira makao makuu ya Alassane Ouattara yaliyo kwenye hoteli ya Golf mjini humo.

Kwa wiki kadhaa sasa, vikosi vya Gbagbo vimeizingira hoteli hiyo na Gbagbo amekataa kuviondosha licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Umoja wa Mataifa, na mwenyewe kuahidi mara mbili kwamba angeliviondoa.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mauaji ya maangamizi na uhalifu dhidi ya binaadamu nchini humo, ikiwa mgogoro huu haukuzuiwa haraka.

Odinga atoka mikono mitupu

Kiongozi anayetambuliwa kama mshindi wa uchaguzi wa Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga
Kiongozi anayetambuliwa kama mshindi wa uchaguzi wa Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Kenya, Raila OdingaPicha: AP

Mapema hapo jana, mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika katika kutafuta suluhu ya Cote d'Ivoire, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alitoka mikono mitupu katika ziara yake ya mwisho nchini humo, baada ya kuambiwa na utawala wa Gbagbo, kwamba asikanyage mguu wake tena Abdijan.

"Bwana Odinga amefeli kwenye ujumbe wake na hatuko tayari kumpokea tena hapa Cote d'Ivoire. Tunamkataa moja kwa moja." Alseima Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Gbagbo, Alcide Djedje.

Odinga mwenyewe alishatangaza tangu jana kwamba, hakuna uwezekano wowote wa Gbagbo kuondoka madarakani kwa hiari yake, kwani amekuwa akivunja kila ahadi anayoiweka, ikiwemo ile ya kuondoa vizuizi kwenye makao makuu ya Ouattara.

"Licha ya majadiliano ya kina na Bwana Laurent Gbagbo na Rais mteule Alassane Ouattara, ambayo yaliendelea mpaka usiku wa manane, nasikitika kutangaza kwamba ule uwezekano uliotarajiwa kuutatua mzozo huu, haukufanikiwa." Alisema Odinga.

Hii ilikuwa ni safari ya pili kwa Odinga mjini Abdijan, na mara hii alikuwa amemwendea Gbagbo na ahadi ya kinga na ulinzi, ikiwa angelikubali kuondoka madarakani, ili kuinusuru nchi isiingie kwenye machafuko zaidi, ambayo hadi sasa yameshasababisha vifo kadhaa vya watu.

Maandalizi ya Operesheni ya Kijeshi

Uamuzi huu wa sasa wa Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi hawa 2,000, ambao unaifanya idadi ya wanajeshi wa kikosi cha UNOCI kufikia 11,500, umekuja katika wakati ambao, wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika ya Magharibi, walikuwa wanakutana nchini Mali, kupanga mikakati ya mwisho ya kumuondoa madarakani Gbagbo kwa kutumia nguvu.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kijeshi wanasema kwamba, ili uvamizi huu wa ECOWAS uwe na mafanikio, ni lazima ushirikishe, kwa uchache, wanajeshi 20,000, ingawa hadi sasa jumuiya hii ina wanajeshi 3,500 tu katika akiba yake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi