1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa wapendekezwa uwajibike Irak

23 Septemba 2007

Mazungumzo yaliyo hudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu kuhusu mustakabali wa Irak yamemalizika katika baraza kuu la umoja wa mataifa mjini New York nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/CB13
Ban Ki Moon katibu mkuu wa umoja wa mataifa
Ban Ki Moon katibu mkuu wa umoja wa mataifaPicha: DW

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon alieongoza mazungumzo hayo pamoja na waziri mkuu wa Irak Nouri Al Malik amesema kwamba licha ya umoja wa mataifa kupendekezwa uwajibike kwa kiwango kikubwa nchini Irak lakini ipo haja ya kuimarisha hali ya usalama nchini humo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice akiwahutubia waandishi wa habari baada ya kumalizika mkutano huo amesema kwamba mazungumzo yataendelezwa kuhusu azimio jipya la baraza la usalama la umoja wa mataifa nambari 1770 linalohusu kikosi cha umoja wa mataifa cha usaidizi nchini Irak kitakacho kuwa na jukumu la kuishauri serikali ya Irak katika maswala mbali mbali.

Irak na nchi majirani zake zilihudhuria mkutano huo pamoja na nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa,Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Canada, Japan na Italia. Umoja wa mataifa pia umepewa jukumu la kufanikisha maridhiano nchini Irak na kuanzisha mazungumzo kati ya nchi hiyo na majirani zake ili kutafuta suluhisho la mipaka yake,misaada ya kibinadamu na jinsi ya kurejea nyumbani takriban wakimbizi milioni 4.5 wa Irak.