1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa warefusha jukumu la kulinda amani Kongo

Zainab Aziz
1 Aprili 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mabli na kurefusha jukumu la kulinda amani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia linaazimia kupunguza idadi ya wanajeshi wake wa kulinda amani nchini humo.

https://p.dw.com/p/2aU8f
UN Mission UNMIL
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Kura iliyopigwa jana inaazimia kupunguza idadi ya wanajeshi hao hadi kufikia 16,200.  Hatua hiyo imefikiwa ijapokuwa imepingwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu - ICC ambayo inachunguza uhalifu wa kivita katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2014. Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda mgogoro wa hivi karibuni pamoja na kuuwawa kwa wataalamu wawili wa kigeni wa Umoja wa Mataifa, ni wazi kuwa uhalifu wa kivita umetendeka.

Hadi watu 400 wameuwawa kutokana na kuendelea kwa mapigano yaliyoanza mwezi Agosti mwaka uliopita wakati majeshi ya serikali yalipomuuwa kiongozi mmoja wa kikabila aliyekuwa anampinga rais Joseph Kabila. Bibi Bensouda ameelezea wasiwasi wake kutokana na ripoti mbalimbali juu ya machafuko mabaya yaliyotokea katika miezi kadhaa iliyopita nchini Kongo na hasa katika jimbo la Kasai. Bensouda ameyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa mjini The Hague. Mwendesha mashtaka huyo mkuu amesema hatasita kuchukua hatua za kisheria na ameapa kuawaadhibu wote wanaohusika.  Jimbo la kati la Kasai, ambako kiongozi wa kikabila Kamwina Nsapu aliuwawa mwaka uliopita, ndio kitovu hasa cha vurugu ambazo zimezagaa hadi katika mikoa mingine jirani ya Kasai-Oriental na Lomami.

Niederlande Den Haag Gerichtsvollzieherin Fatou Bensouda beim Fall Jean-Pierre Bemba
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou BensoudaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Lampen

Utekaji nyara na mauaji

Miili ya watalaamu wawili wa Umoja wa Matafia ilipatikana wiki hii.  Wataalamu hao walikuwa Mmarekani Michael Sharp na Zaida Catalan raia wa Sweden.  Watu hao waliripotiwa kupotea tangu mwanzoni mwa mwezi wa Machi. Mwili mmoja moja kati ya hiyo miwili ulikuwa umeharibika vibaya. Hadi kufikia sasa raia wanne wa Kongo waliokuwa wameandamana na  wataalamu hao bado hawajulikani waliko.  Mabalozi katika Umoja wa Mataifa walisema  wataalamu hao walikuwa wanachunguza taarifa juu ya makaburi ya halaiki.  Wiki iliyopita askari wapatao 39 pia walivamiwa na kuuwawa na waasi katika jimbo hilo la Kasai.

Bensouda amezitolea mwito pande zote kujiepusha na vitendo vya uhalifu wa kivita huku akiitaka serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwafungulia mashtaka waliohusika na mauaji hayo katika taifa hilo la Afrika ya Kati linalokabiliwa na machafuko.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC ilianzishwa mnamo mwaka 2002 kwa ajili ya kuchunguza na hatimaye kuwafungulia mashitaka watu wanaofanya uhalifu mbaya duniani. Uchunguzi wao katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umewezesha kuwafikisha watuhumiwa katika mahakamna hiyo ya kimataifa ya ICC na tayari hukumu zimeshatolewa katika kesi mbili.

Mbabe wa kivita Thomas Lubanga  alihukumiwa kifungo cha miaka 14 kutokana na kuwatumikisha watoto katika jeshi lake la waasi na Germain Katanga alifungwa miaka 12 kwa kuhusika na mapigano ya kikabila ya mwaka  2003 katika kijiji kimoja kwenye mkoa wa Ituri uliopo kaskazini mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Kesi ya mtuhumiwa wa tatu Bosco Ntaganda bado inaendelea. Ntagamba anakabiliwa na tuhuma18 za uhalifu wa kivita pamoja nakuwatesa binadamu. Mtuhumiwa huyo amekanusha tuhuma hizo dhidi yake lakini waendesha mashtaka wanasema alihusika na alikuwa kiungo cha kati katika machafuko ya Ituri.  Watu wapatao 60,000 wameuwawa tokea mwaka 1999, kwa mujibu wa taarifa za makundi ya kutetea haki.

Umoja wa Mataifa unamshinikiza rais Joseph Kabila kuheshimu makubaliano ya kugawana madaraka na upinzani kablaya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu. Lakini mpaka sasa haijulikani iwapo rais Kabila ataachia madaraka mwaka huu. Umoja wa mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wamehimiza kutajwa kiongozi mpya wa upinzani kulingana na makaubaliano yaliyofikiwa mwezi desemba mwaka uliopita.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/d.w/p/2a/TW3

Mhariri: Sudi Mnette