1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wasifu kupungua mashambulizi ya maharamia Somalia

24 Oktoba 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa limesema kuimarishwa kwa ulinzi wa kutumia meli Somalia kumesaidia kupunguza wimbi la mashambulizi ya maharamia nchini humo .

https://p.dw.com/p/1A5jA
Picha: Reuters

Ripoti ya Katibu mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-Moon, imeonyesha kuwa kumetokea mashambulizi 17 tu mwanzoni mwa mwaka huu, ikilinganishwa na mashambulizi 99 yaliyofanywa mwaka jana mwanzoni.

Mpaka Oktoba 17 mwaka huu ni meli moja tu ndogo yenye abiria 60 ambayo bado inashikiliwa na maharabia, wengi wao wakiwa hawajulikani na maharamia hao kuendelea kuneemeka ambapo mwaka jana walikusanya hadi bilioni 40 za Marekani kama fidia ya kuwaachia huru mateka.

Huku hayo yakiendelea na Somalia ikifanya mchakato wa kujijenga upya baada ya miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na kile kinachoelezwa kuwa mfumo mbaya wa sheria tangu kupinduliwa madarakani kwa Rais Siad Barre wa nchi hiyo mwaka 1991, Umoja wa Mataifa umetaka kuimarishwa zaidi kwa ulinzi.

Hata hivyo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ripoti hiyo amelaumu kitendo cha maharamia hao kuwateka kwa muda mrefu na kuwatesa watu wasio na hatia na kuwatishia ikiwa hawataweza kutoa kiasi kikubwa cha fedha wanachotozwa ili kuachiwa huru.

Dola milioni 40 zatozwa kama fidia kuwaachia mateka

Makadirio ya ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia dawa za kulevya na makosa ya jinai na yale ya Benki ya Dunia yanaonyesha kuwa maharamia nchini Somalia walipokea hadi dola milioni 400 za Marekani kati ya Aprili 2005 hadi Desemba 2012 kama fidia ili kuwaachia mateka.

Symbolbild Frauen Vergewaltigung Not Hunger Armut in Somalia
Wakimbizi kutoka Somalia wakisubiri kuandikiswa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, KenyaPicha: Oli Scarff/Getty Images

Ingawa uvamizi wa jeshi maalumu la wanamaji uliofanywa na Marekani mwaka 2009 dhidi ya maharamia, ulididimiza kasi ya maharamia wa Somalia kudai malipo ya fidia, wakati ambapo mmoja wa maharamia aliyetiwa nguvuni anaendelea kutumikia kifungo nchini Marekani

Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema suala la maharamia wa Somalia halitiliwi mkazo na serikali ya Somalia wala mamlaka husika, ambao hawajafanya uchunguzi wa kina kuhusu kinachoendelea juu ya maharamia hao.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo amesema ameguswa na suala la kuimarishwa kwa ulinzi nchini Somalia na kuahidi ushirikiano zaidi kutoka jumuiya ya kimataifa ili kukabiliana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye mafungamano na magaidi wa Al-Qaeda.

Bomu lauwa 16 kwenye mgahawa

Huku hayo yakiarifiwa kwa upande mwingine washambuliaji wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab wanaendelea na mashambulizi.

Mapigano bado yanaendelea Somalia, ambapo wiki iliyopita bomu lenye sumu liliripuliwa na kuua takriban watu 16 katika mgahawa mmoja uliopo karibu na mpaka wa Ethiopia, eneo ambalo mara nyingi mapigano baina ya askari wa kigeni na wanajeshi wa Al-Shabaab yanaendelea.

Jambo ambalo Ban Ki Moon ameonya kwamba ni kielelezo tosha namna magaidi wa kundi la Al-Shabaab, ambao hivi karibuni walifanya shambulio dhidi ya jengo la maduka la Westagate mjini Nairobi Kenya na kusababisha maisha ya watu zaidi ya 60 kuangamia, walivyojipanga kufanya mashambulizi na kutishia usalama Somalia na maeneo mengine.

Ban Ki-moon New York 27.09.2013 Overlay
Katibu mkuu wa Umoja wa Mtaaifa Ban Ki-moon aahidi kuongeza majeshi ya kulinda amani SomaliaPicha: picture alliance/abaca

Kufuatia hali hiyo, Ban Ki-Moon amesema kunahitajika hatua za haraka za kuimarisha ulinzi wa kijeshi dhidi ya Al-Shabaab na kurejea makubaliano ya awali dhidi ya kuongezwa kwa wanajeshi kufikia 2,550 kutoka wanajeshi elfu 20,000 wa awali na kuongezwa muda wa ulinzi kwa hadi miaka miwili zaidi.

Mwandishi: Flora Nzema/RTRE

Mhariri: Josephat Charo