1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa watahadharisha dhidi ya kuwabughudhi wakimbizi wa Somalia.

Sekione Kitojo23 Julai 2010

Umoja wa mataifa umesema kuwa wakimbizi kutoka Somalia wanabughudhiwa na kukamatwa nchini Kenya pamoja na jimbo lilijitangazia uhuru la Somalia la Puntland.

https://p.dw.com/p/OTAv
Familia ya Kisomali ikihamisha vyombo kwa kutumia mkokoteni unaokokotwa na punda wakati wakiukimbia mji wa Mogadishu.Picha: AP

Umoja  wa  mataifa   umesema  leo  kuwa  wakimbizi kutoka  Somalia  wanabugudhiwa  na  kukamatwa  nchini Kenya  pamoja  na  jimbo  lililojitangazia  uhuru  la  Somalia la Puntland  kutokana  na  shambulio  la  bomu  lililofanywa na  kundi  la  Waislamu  wenye  msimamo  mkali  la  al-Shabaab  nchini  Uganda. hayo  ameyasema  msemaji  wa shirika  la  umoja  wa  mataifa  la  kuwahudumia  wakimbizi, UNHCR, Melissa Fleming  mjini  Geneva.

Maafisa  katika  jimbo  la  Puntland wamewarejesha  katika maeneo  ya   mzozo  katikati  ya  Somalia  wiki  hii   zaidi ya  Wasomali  900  ambao  wamekimbia  makaazi  yao, lakini   hadi  sasa  Kenya  haijawarejesha  Wasomali ambao  wanaweza  kuthibitisha   kuwa  wana  hadhi  ya ukimbizi, amesema  kamishna  wa  shirika  la   umoja  wa mataifa   la  kuwahudumia  wakimbizi.

Kutokana  na  mashambulio  ya  kigaidi   hivi  karibuni, tumegundua  matukio  kadha  ya  kibaguzi  dhidi  ya wageni, kukamatwa  na  kurejeshwa   makwao  Wasomali ambao  wamekimbia   mapigano, Melissa Fleming, msemaji wa  wa  UNHCR, amewaambia  waandishi  habari  mjini Geneva.

Tunatoa  wito  kwa  maafisa  wa  jimbo  la  Puntland kusitisha  hatua  hizi  za  kuwarejesha  wakimbizi, ameongeza.

Watu  wanaokimbia  mapigano  kusini  na  kati  ya  Somalia wanahitaji  ulinzi  wa  kimataifa   na  kulazimishwa  kurejea katika  maeneo  hayo  kunaweka  maisha  yao  katika  hali ya  hatari  kubwa, kwa  mujibu  wa  msemaji  huyo  wa umoja  wa  mataifa. Tunahofia  kuwa  wale  ambao wamekimbia  wakiwa  na  sababu  muhimu , vijana   katika umri  wa  miaka   kati  ya  18  na  25, mara  nyingi wanalengwa  katika  kuingizwa  katika  makundi  ya wapiganaji  kama  al-Shabaab, Fleming  amesema.

Al Shabaab , kundi   la  waasi  wa  Kiislamu  lenye msimamo  mkali  wa  kidini  likiwa  na  uhusiano  na  kundi la  al Qaeda, linadhibiti  sehemu  kubwa  ya  kusini  mwa Somalia , inayopakana  na   kaskazini  mashariki  ya Kenya, na  linapigana   kutaka  kuiangusha   serikali inayoungwa  mkono  na  mataifa  ya  magharibi  katika taifa hilo  lililoko  katika   pembe  ya  Afrika.

Wapiganaji  wa Kiislamu  nchini   Somalia  wamewauwa wanajeshi  wawili  wa  jeshi  la  kulinda  amani  la  Afrika , katika  mji  mkuu  Mogadishu, amesema  msemaji  wa ujumbe  wa  umoja  wa  Afrika  wa  kulinda  amani  leo Ijumaa.

Wakati  huo  huo  wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya Marekani  imetoa  tamko  la  tahadhari  ya  kusafiri  jana Alhamis  kwa  raia  wa  Marekani  wanaotaka  kwenda Kenya, ikielezea  kuhusu  kuongezeka  kwa   kitisho kutokana  na  shambulio  la  bomu  la  kujitoa  muhanga mapema  mwezi  huu  katika  nchi  jirani  ya  Uganda.

Ubalozi  wa  Marekani  katika  mji  mkuu  wa  Kenya, Nairobi  umewataka  raia  wa  Marekani   kuchukua tahadhari    wawapo  katika  maeneo  ya  watu  wengi  na kuwaonya  kuepuka kufika  katika  mikutano  ya  hadhara na  maandamano.

Wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Marekani  pia  imeonya kuhusu  uwezekano  wa  kutokea   ghasia  wakati  wa kukaribia  kura  ya  maoni  kuhusu  katiba  mpya  nchini Kenya.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / RTRE

Mhariri :