1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka machafuko ya Myanmar kusitishwa

John Juma
14 Septemba 2017

Katibu wa Umoja wa Mataifa amesema kampeni ya kijeshi ni sawa na takasataka ya kikabila dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

https://p.dw.com/p/2jxAH
Bangladesch Flüchtlingslager Kutupalong
Picha: Getty Images/AFP/M. Uz Zaman

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limevunja kimya chake kirefu kuhusu mgogoro wa nchini Myanmar na kutoa wito wa kukomesha vurugu, huku Katibu wa Umoja wa Mataifa akisema kampeni ya kijeshi ni sawa na takasataka ya kikabila dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Wakati huohuo, shirika la habari la serikali ya Myanmar limesema China imeunga mkono hatua za jeshi la Myanmar dhidi ya wapiganaji wa Rohingya.

Kwa mara ya pili, Baraza la Usalama lenye wanachama kumi na tano lilikutana faraghani kujadili mzozo wa Myanmar na wakakubali kwa pamoja kulaani hali hiyo hadharani. Tekeda Alemu, rais wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa amesema: "Baraza limeelezea wasiwasi kuhusu ripoti za matumizi ya vurugu kupita kiasi wakati wa operesheni za usalama, na kutaka usitishwaji wa mara moja wa machafuko hayo ili irudishe hali ya kawaida ya kuzingatia sheria, kuhakikisha raia wanalindwa na kusuluhisha tatizo la wakimbizi."

Changamoto kuu kwa Aung San Suu Kyi

Myanmar Aung San Suu Kyi Rede vor der UN Vollversammlung in New York 2016
Picha: Reuters/C. Allegri

Machafuko ya Rakhine na kukimbia kwa maelfu ya wakimbizi, ni changamoto kubwa kuwahi kumkabili kiongozi wa Myanmar ambaye pia ni mshindi wa tuzo la Amani Aung San Suu Kyi tangu awe kiongozi wa taifa hilo mwaka uliopita.

Mapigano hayo yalianza kufuatia misururu ya mashambulizi ya wanamgambo wa Rohingya dhidi ya vituo vya kiusalama mnamo Agosti 25, ambapo watu kadhaa waliuawa. Abdul Goffar ambaye ni mmoja kati ya wakimbizi wa Rohingya anaelezea masaibu yaliyowakumba: "Wakati wanajeshi na polisi walipokizingira kijiji chetu na kutushambulia kwa maroketi kuwasha moto, tulikimbia kutoka kijiji chetu na kuelekea kokote kule tulikoweza kwenda."

Hata hivyo balozi wa China nchini Myanmar Hong Liang amenukuliwa leo na gazeti la Global New Light la Myanmar akiwaambia maafisa wakuu wa serikali kuwa "Msimamo wa China kuhusu mashambulizi ya kigaidi katika jimbo la Rakhine ni wazi, ni suala tu la ndani ya nchi" na hatua ya walinda usalama wa Myanmar dhidi ya magaidi wenye misimamo mikali pamoja na hatua za serikali kutoa misaada kwa watu zinaungwa mkono kikamilifu.

Suu Kyi anatarajiwa kuhutubia taifa siku ya Jumanne. Wakosoaji wametaka apokonywe tuzo la amani kwa kushindwa kumaliza machafuko ambayo pia yamehusisha uteketezaji wa vijiji na kusababisha Warohingya Waislamu 380,000 kukimbilia Bangladesh.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/DPAE

Mhariri:Iddi Ssessanga