1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa watoa ripoti kuhusu hali ya kijamii duniani

Josephat Charo29 Novemba 2007

Umoja wa Mataifa unasema katika ripoti yake kwamba biashara huru, ubinafsishaji na utandawazi unawazuia watu wengi kunufaika kutokana na elimu na raslimali.

https://p.dw.com/p/CUQy

Dunia ina raslimali, utajiri na elimu kuweza kuifanya hali nzuri ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni kuwa haki msingi kwa wote. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kijamii duniani iliyotolewa Jumatatu wiki hii.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kijamii, inayotolewa baada ya kila miaka miwili, inasema kufurahia raslimali, utajiri na elimu kama haki msingi kunafanyika tu miongoni mwa baadhi ya watu wa matabaka fulani.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na idara ya uchumi na maswala ya jamii ya Umoja wa Mataifa inasema mamilioni ya watu ulimwenguni kote hawana ajira kwa sababu ya athari zinazosababishwa na biashara huru, ubinafsishaji na utandawazi.

Johan Scholvinck, mkurugenzi wa idara ya uchumi na maswala ya jamii ya Umoja wa Mataifa, DESA, amesema manufaa ya biashara huru na utandawazi huwaendea watu walio na ujuzi mwingi na walio na elimu nzuri katika ulimwengu huu wa utandawazi.

Akitoa mfano wa uhamiaji wa kimataifa, mkurugenzi huyo amesema ni rahisi kwa mtu mwenye elimu nzuri kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine, kupata kazi yenye mshahara mzuri. Lakini mtu asiye na elimu, hukabiliwa na matatizo mengi mno.

Tatizo kubwa ni ukosefu wa ajira, ambalo katika muongo mmoja uliopita limeongezeka kwa idadi ya watu milioni 34, hadi kufikia milioni 195 mwaka jana. Kati ya idadi ya watu wasio na ajira, nusu ni vijana, ingawa wanawakilisha asilimia 20 ya idadi ya wakaazi duniani.

Ripoti hiyo inasema kulazimishwa kufanya mambo kunakosababishwa na ukosefu wa elimu na jutojua kusoma na kuandika, ni sababu kubwa ya idadi hii kubwa.

Wakati huo, watoto milioni 190 chini ya umri miaka 14 wanafanya kazi fulani. Asilimia 25 kati yao wanaishi barani Afrika kusinu mwa jangwa la Sahara, lakini takriban asilimia 70 wanaishi katika maeneo ya Asia na Pacific.

Sha Zukang, naibu katibu mkuu anayehusika na maswala ya kiuchumi na kijamii, amesema kuna wasiwasi kuhusu mienendo duniani kote. Licha ya ukuaji wa kiuchumi, kutengeza nafasi za ajira kunakosekanakutokana na kuonezeka kwa idadi ya wafanyakazi wazee.

Kutoka mwaka wa 1996 hadi 2006 pato la dunia likukua kwa asilimia 3.8, lakini katika muongo huo huo ukosefu wa ajira uliongezeka kutoka asilimia 6 hadi 6.3.

Mkurugenzi wa kitengo cha sera ya jamii na maendeleo cha idara ya uchumi na maswala ya jamii ya Umoja wa Mataifa, DESA, Johan Scholvinck, amesema wanaonufaika kutokana na utandawazi pia hupokea mishahara minono.

Kasi kubwa ya ukosefu wa ajira iligunduliwa huko Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Ikilinganishwa na mwaka wa 1996, idadi ya watu wasio na ajira ilipungua kwa asilimia 0.8, lakini asilimia 12.2 wanalazimika kuishi bila mshahara wa kutegemewa.

Kwa mujibu wa Zukand, ukuaji wa kiuchumi na ajira hayaendi sambamba hivyo kuziathiri jamii na wananchi. Wakati huo huo mazingira ya kazi yanaendelea kuwa mabaya. Kuna wasiwasi mkubwa wa ukosefu wa usalama wa ajira miongoni mwa wafanyakazi wengi.

Makundi ya wafanyakazi yanakabiliwa na wasiwasi kwa sababu ya hatua zinazochukuliwa na waajiri duniani kote kuongeza mabadiliko katikysoko la ajira.

Scholvinck amesema hii ni kwa sababu imekuwa vigumu zaidi kwa serikali kugharamia mipango fulani ikiwemo ukosefu wa ajira, bima, malipo ya uzeeni na mingine mingi. Serikali zinafuharia mipango ambapo wafanyakazi wanalipia malipo yao ya uzeeni na bima ya afya.

Takriban nusu na idadi ya watu wasio ajira ulimwenguni ni sehemu ya kundi la watu wanaofanya kazi wapate dola mbili kwa siku. Huku idadi hii ikisemekana ilikuwa juu mnamo mwaka wa 1966, mwaka jana wafanyakazi milioni 1.4 hawakuweza kujipatia fedha kujikwamua kutokana na umaskini na kupata zaidi ya dola mbili kwa siku.

Naibu katibu mkuu anayehusika na maswala ya kijamii na kiuchumi, Sha Zukang, amesema hii ndio sababu kwa nini ripoti ya sasa ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kijamii imezingatia sana ajira kama swala lenye umuhimu mkubwa kwa nchi zote duniani, kwa jukumu kubwa la kupunguza umaskini.