1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa yashindwa kutatuwa mzozo wa Kosovo

20 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CdwH

NEW YORK

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana limeshindwa kuondowa kikwazo juu ya mzozo wa mustakbali wa Kosovo ambapo mabalozi wanasema mazungumzo zaidi kati ya wahusika yatakuwa hayana maana na kwamba msimamo wa hali iliopo hivi sasa kwenye jimbo hilo la Serbia lililojitenga haiwezi kuendelea milele.

Akizungumza kwa niaba ya nchi wanachama wa mataifa ya magharibi kwenye baraza hilo Balozi wa Ubelgiji Johan Verbeke ambaye ni msemaji wa Umoja wa Ulaya amesema maelezo yaliyotolewa na viongozi wa Serbia na Wakosovo wa asili ya Albania walio wengi kwenye jimbo hilo kumethibitisha kwamba maoni yao bado hayawezi kusuluhishwa.

Verbeke anasema ni wazi kwamba mazungumzo zaidi kwa njia hii au mfumo mwengine wowote ule hayawezi kuleta mabadiliko yoyote yale.

Hata hivyo Serbia ikiungwa mkono na Urusi ambayo ina matumaini kwamba mazungumzo hayo yanaweza kuendelea na kutowa matokeo yatakayokubalika na pande zote mbili zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono mazungumzo zaidi.

Nchi wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamekutana katika mkutano wa faragha kusikiliza hoja za Waziri Mkuu wa Serbia Vojislau Kostunica na Rais wa Kosovo Fatmir Sejdiu.

Kushindwa kufikia muafaka katika Umoja wa Mataifa kunaweza kupelekea Serbia kujitangazia uhuru.