1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UMOJA WA MATAIFA:Makundi ya waasi wa Sudan kushawishiwa kuhudhuria mkutano

25 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Cr

Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa linatoa wito kwa makundi yote ya waasi wa Sudan kuhudhuria mkutano wa kutafuta amani unaopangwa kufanyika jumamosi.Mkutano huo unawaleta pamoja waasi na wawakilishi wa serikali ukiwa na lengo la kumaliza ghasia katika eneo la Darfur la Sudan zilizodumu miaka minne u nusu.Baraza hilo linatisha kuchukulia hatua upande wowote utakaohujumu juhudi za kutafuta amani katika eneo hilo.Katika taarifa yake iliyosomwa hapo jana kwenye mkutano rasmi,Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linasisitiza umuhimu wa kufikia makubaliano ya kisiasa katika eneo la Darfur yatakayoshirikisha wahusika wote.Hatua ya kwanza ni kusitishwa kwa mapigano jambo litakalosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Afrika. Jan Eliasson ni mjumbe wa Umoja wa mataifa katika Darfur

''Kumeendelea kuwa na mgawanyiko katika serikali.SPLM waliamua kujiondoa bungeni jambo linalolazimu mabadiliko ya mtizamo wa kisiasa nchini Sudan.Hali halisi imebadilika ila sharti tuendelee na juhudi za kutafuta amani.Ninataraji kuwa katika kipindi cha siku zijazo mambo yatabadilika. ''

Baraza hilo halijafafanua hatua itakazoichukua endapo hilo halitimizwi ila huenda ikajumuisha hatua ya kuwekewa vikwazo.Serikali ya Sudan kwa upande wake inasema kuwa itatangaza hatua ya kusitisha vita kabla kuanza kwa mazungumzo hayo ya Sirte nchini Libya.Hata hivyo haijulikani iwapo waasi watachukua hatua hiyo kwani wengi ya makundi hayo yanasusia mazungumzo hayo.