1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa:MONUC kubakia Kongo

16 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC1f

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha jeshi la MONUC kuendelea kubakia katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mpaka ifikapo mwisho wa mwaka.Baraza hilo lililo na nchi wanachama 15 liiidhinisha azimio hilo linalotoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja Wa Mataifa Ban Ki Moon kutoa ratiba ya kikosi hicho kuondoka kwa awamu ifikapo katikati ya mwezi Novemba.Ujumbe wa MONUC ulio na wanajeshi alfu 17 ndio mkubwa kabisa wa Umoja wa Mataifa kote ulimwenguni.Muda ulioongezwa unamalizika Disemba 31 mwaka huu.

Rais Joseph Kabila alishinda katika uchaguzi mkuu mwaka jana mwezi Oktoba uliolenga kurejesha amani katika taifa tatu kwa ukubwa barani Afrika kufuatia kipindi cha vita vilivyodumu kuanzia mwaka 98 hadi 2003.Vita hivyo vilisababisha vifo vya watu takriban milioni 4 waliopata maambukizi vilevile kukumbwa na njaa.

Jeshi la MONUC lilianza shughuli zake katika eneo lililo na madini mengi mwaka 99 huku wanajeshi 98 wa kulinda amani wamepoteza maisha yao mpaka sasa.

Azimio hilo jipya linalenga kuimarisha majukumu ya MONUC ili kutimiza mahitaji mapya ya Kongo inapojiandaa katika ukarabati wa nchi.

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unatazamiwa kuenda nchini Kongo mwezi ujao ili kusimamia mpango huo mpya.