1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kujadilia mzozo wa Kaukasus

1 Septemba 2008

Maandamano yapangwa kulaani hatua za Urusi katika Georgia.

https://p.dw.com/p/F8Qu
Rais Nikolas Sarkozy (Kushoto) alipokutana na Dmitry Medvedev wa Urusi mjini Moscow tarehe 12 Agosti 2008 katika jitihada za kuutanzua mgogoro wa maeneo ya Georgia ya Ossetia kusini na Abkhazia.Picha: AP

Kabla ya kikao hicho leo mjini Brussels, Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye nchi yake ndiyo mwenyekiti wa umoja huo hivi sasa, wadhifa unaozunguka miongoni mwa wanacahama baada ya kila miezi sita, alikuwa na mazungumzo kwa simu jana na Rais wa Urusi Dimitry Medvedev.

Inaripotiwa walizungumzia juu ya eneo lililoundwa na majeshi ya Urusi ndani ya Georgia katika kile yanachodai kuwa ni eneo la kuzitenganisha Georgia na mahasimu wake Ossetia kusini na Abkhazia zinazotaka kujitenga .

Ingawa Ikulu mjini Moscow haikutoa maelezo yoyote juu ya mazungumzo hayo,baadae Waziri mkuu wa Ufaransa Francois Fillon alikiambia kituo cha matangazo ya redio Europe nambari moja kwamba Rais Sarkozy binafsi yuko tayari kwenda katika miji mikuu ya Urusi na Georgia - Moscow na Tibilisi - kujaribu kuutatua mgogoro huo.

Mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya wa wanachama 27 unafanyika huku ukiwa umegawika kuhusiana na suala la vikwazo dhidi ya Urusi. Baadhi ya nchi zina wasi wasi kwamba Urusi inaweza kutumia mafuta na gesi inayosafirisha hadi nchi za ulaya, kulipiza kisasi ikiwa hatua kali zitachukuliwa na mataifa ya umoja huo dhidi yake. Rais Medevedev alionya hivi karibuni kuwa nchi yake sio itakayoathirika.

Pamoja na hayo kuna msukumo kutoka kwa mataifa ya ulaya mashariki kutaka pazingatiwe yafuatayo:

1.Kuahirishwa au kufutwa duru ijayo ya mazungumzo juu ya mkataba mpya wa ushirikiano kati ya Urusi na Umoja wa ulaya yaliopangwa kufanyika tarehe 15-16 ya mwezi huu

2.Kuweka masharti makali kwenye utaratibu wa visa kwa Warusi

3.Na kutoiunga mkono katika juhudi zake kutaka kujiunga na shirika la biashara duniani WTO.

Akizungumzia msimamo wa nchi yake na nini Umoja wa Ulaya unachoweza kufanya Waziri mkuu wa Georgia Lado Gurgenize aliiambia Deutsche Welle kuwa,"Umoja wa ulaya unaweza kufanya mengi, kuanzia kutuma ujumbe wa waangalizi wa kiraia na wakaguzi, na hatimae kuongoza utaratibu wa uwekaji na usimamiaji amani wa kimataifa, ambao utachukua nafasi ya majeshi ya Urusi."

Rais Sarkozy kwa upande wake amependekeza dondoo sita za makubaliano yalioandaliwa na Umoja wa ulaya ambazo ni pamoja na kuondoshwa kwa vituo vya ukaguzi vya Warusi katika ardhi ya Georgia, kurudi nyuma kwa majeshi hayo hadi sehemu yalikokuweko kabla ya mgogoro kuzuka na mazungumzo ya kimataifa kuhusu mfumo wa usalama na utulivu katika Ossetia kusini na Abkhazia.

Wakati huo huo maandamano yamepangwa kufanyika kote nchini Georgia kupinga hatua za Urusi na kuendelea kuwepo majeshi yake ndani ya ardhi ya Urusi, ambapo Warusi wanasema wanasimamia amani. Maandamano pia chini ya kauli mbiu "Zuwia Urusi " yamepangwa pia kufanyika katika miji mikuu ya nchi kadhaa za Ulaya.