1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuongeza vikwazo kwa Urusi

Elizabeth Shoo9 Septemba 2014

Maafisa wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuiwekea Urusi vikwazo zaidi kufuatia shutuma kwamba nchi hiyo inahusika kwenye mgogoro unaoendelea Mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1D9Bu
Jengo la kamisheni kuu ya Umoja wa Ulaya
Picha: cc-by-sa/TPCOM

Umoja wa Ulaya umeamua kuuchelewesha muda wa kuanza vikwazo dhidi ya Urusi ili kuangalia iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano yataheshimiwa. Awali mpango wa Umoja wa Ulaya ulikuwa kuvipitisha vikwazo hivyo ili vianze Jumanne, lakini baadhi ya nchi, ikiwemo Finland, zilikataa, zikiitaka Urusi ipewe muda zaidi.

Vikwazo hivyo vitauathiri hasa uchumi wa Urusi. Mwenyekiti wa baraza kuu la Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy, ametangaza kwamba makampuni makubwa ya Urusi, yakiwemo yale yanayouza mafuta na silaha, hayataruhusiwa kufanya biashara kwenye soko la fedha la Ulaya. Pamoja na hayo, Umoja wa Ulaya utawawekea vikwazo vya kusafiri wale wote wanaoonekana kuchochea mapigano Ukraine au wanaoaminika kumshawishi rais Vladimir Putin katika sera zake zinazoihusu Ukraine.

Malaysia Airlines ilivunjika angani

Lakini waziri mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev ameuonya Umoja wa Ulaya kwamba vikwazo hivyo vikiidhinishwa basi mashirika ya ndege ya Ulaya hayataruhusiwa kurusha ndege zake kwenye anga ya Urusi. Ingawa wanajeshi wa Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga wamekubaliana kuweka silaha zao chini, hali ya usalama mashariki mwa Ukraine bado ni tete. Kumekuwa na ripoti za mapigano kwenye mji wa Donetsk ambao ni moja ya ngome kuu za waasi. Hapo jana rais Petro Poroshenko wa Ukraine aliutembelea mji wa Mariupol ambao umeshuhudia mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi. "Tuna uwezo wa kuitetea nchi yetu. Tuna uwezo wa kuutetea mji huu. Suala la muhimu zaidi sio makombora, vifaru au wanajeshi wenye silaha. Suala la msingi ni moyo wa watu hawa, moyo wa raia wa Ukraine. Sisi tuna moyo wa kishujaa kwa sababu tunaitetea nchi yetu," alisema Poroshenko.

Premierminister Medwedew zu Besuch auf der Krim
Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry MedvedevPicha: Reuters

Katika tukio jengine, baraza la usalama la uholanzi limetoa ripoti yake juu ya ajali ya ndege ya Malaysia Airlines MH17 iliyoanguka kwenye ardhi ya Ukraine. Uchunguzi wa awali unathibitisha kuwa ndege hiyo ilishambuliwa na vifaa vilivyokuwa vikitembea kwa kasi kubwa na hivyo kuifanya ndege hiyo ivunjike na kuanguka. Lakini bado haifahamiki iwapo waasi waliidungua ndege hiyo au kama ajali ilisababishwa na makombora ya jeshi la Ukraine.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/afp/ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman