1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kusaidia waasi Syria

Carolyne Robi23 Aprili 2013

Umoja wa Ulaya umekubali kulegeza vikwazo dhidi ya Syria ili kuruhusu waasi nchini humo kuuza mafuta katika hatua inayonuiwa kuwapa waasi hao uwezo wa kifedha.

https://p.dw.com/p/18LAq
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wakijadili kuwasaidia waasi Syria
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wakijadili kuwasaidia waasi SyriaPicha: GEORGES GOBET/AFP/Getty Images

Uamuzi huo ulioafikiwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya hapo jana huko Luxembourg utawaruhusu wanunuzi kutoka bara Ulaya kununua malighafi ya mafuta kutoka Syria ilimuradi ununuzi huo umeidhinishwa na upande wa upinzani wa Syria. Vikwazo hivyo viliwekwa mwaka 2011 ili kupunguza makali ya ukandamizaji wa Rais Bashar Al Assad dhidi ya waandamanaji waliotaka mageuzi ya uongozi.

Maafisa hao wa Umoja wa Ulaya wamesema kulegezwa huko kwa masharti kutafuatwa na msaada zaidi na uungwaji mkono kwa waasi huku kukiwa na hofu ya kuwepo kwa janga la kibinadaamu kote nchini humo. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo, Catherine Ashton, amesema hali ya kibinaadamu imefikia viwango vya kuogofya na ndiposa baraza hilo la mawaziri liliafikia uamuzi wa kuruhusu upinzani nchini Syria kuuza mafuta yaliyo katika maeneo wanayoyadhibiti.

Kuna changamoto ya kununua mafuta

Ununuzi wa malighafi hiyo kutoka Syria itakuwa vigumu kutokana na sababu za kiusalama na miundo mbinu mibovu lakini maafisa wa umoja wa ulaya wamesema usadizi zaidi wa kifedha utatolewa.Mwanachama mmoja wa ngazi za juu wa upande wa upinzani Syria amesema itachukua takriban mwezi mmoja kabla ya kuweza kuuza mafuta hayo kwani upinzani haina serikali itakayoweza kusimamia biashara hiyo.

Kulingana na takwimu za Marekani,uzalishaji mafuta nchini Syria ulikuwa mapipa elfu 153 kwa siku mwaka jana ikiwa ni pungufu la asilimia 60 ikilinganishwa na mwezi Machi mwaka 2011 wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza.

Maafa ya vita Syria
Maafa ya vita SyriaPicha: Reuters

Hata hivyo Umoja wa Ulaya bado haujaondoa vikwazo vya silaha dhidi ya Syria huku mawaziri hao wa mambo ya nje wakionekana kutofautina kuhusiana na suala hilo la kuwapa waasi usaidizi wa silaha.Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema bado nchi yake haijashawishika kuwapa silaha waasi kwani zinaweza kuishia kwa mikono isiyokusudiwa ya magaidi,msimamo unaonekana kuungwa mkono na Marekani.Uingereza na Ufaransa zimekuwa zikitaka upande wa upinzani upewe silaha.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon hapo jana aliomba kusitishwa kutolewa silaha kwa upande mmoja katika vita vya Syria kwani kutamaanisha vifo na maafa zaidi,jambo ambalo lilipingwa na kiongozi wa Jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil Al Arabi.

Katibu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: AFP/Getty Images

Wakati huo huo kundi la watu waliokuwa na silaha limewateka nyara maaskofu wawili katika jimbo la Aleppo walipokuwa katika shughuli ya kutoa misaada ya kibinadamu katika kijiji kimoja.Walioshuhudia wamesema gari la maaskofu hao lilisimamishwa na dereva kuuwawa na kuwateka nyara maaskofu hao wa kanisa la kiorthodox.

Visa vya utakaji nyara vimeongezeka nchini Syria tangu mapigano kuchacha kati ya waasi na majeshi ya serikali.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo