1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU-Sondergipfel

Miraji Othman20 Novemba 2009

Mbelgiji, rais wa baraza la kudumu la Ulaya, Muengereza waziri wa mambo ya kigeni

https://p.dw.com/p/Kbz0
Herman Van Rompuy, rais wa baraza la kudumu la Umoja wa Ulaya, na Bibi Catherin Ashton, waziri wa mambo ya kigeni wa umoja huo, punde baada ya kuchaguliwaPicha: AP

Wakuu wa serekali na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya jana usiku walikubaliana juu ya watu watakaoshikilia nyadhifa mpya mbili za juu kabisa katika umoja huo. Walimchagua HERMAN VAN ROMPUY kuwa rais wa baraza la kudumu na Bibi Catherine Ashton kuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo.

Ni nafasi ambayo Ulaya imeipoteza. Hayo ni matokeo ya kusikitisha ya mkutano wa jana wa kilele wa Umoja wa Ulaya. Mkataba wa Lisbon ulitoa uwezekano, kupitia cheo cha rais wa baraza la Ulaya, kwamba umoja huo uoneshe sura ilio imara katika nchi za nje. Lakini kwa kuteuliwa Herman Van Rompuy nafasi hiyo haijatumiwa.

Sababu muhimu iliotokana na uamuzi huo sio juu ya nini kile ambacho Umoja wa Ulaya unataka kipate kutokana na wadhifa huo wa kiasiasa, lakini uzito uliwekewa katika uwezekano wa kuwa na wizani, baina ya bawa la la kisiasa la mrengo wa shoto na mrengo wa kulia, baina ya nchi kubwa na ndogo, zile za Mashariki na za Magharibi, zile za Kaskazini na za Kusin, baina ya wanawake na wanaume katika Umoja huo. Hayo yote yalitiliwa maanani katika kuchaguliwa rais wa baraza la kudumu na pia mwakilishi mkuu wa umoja huo katika siasa za kigeni. Ikiwa mtu anataka kufaulu kuzijaza nyadhifa hizo, basi inabidi watu waafikiane katika shuruti ya pamoja. Van Rompuy amekuwa sasa rais wa baraza la kudumu, sio kutokana na sababu kwamba yeye ameonekana kuwa ni mtetezi aliye bora kabisa, lakini kwa vile yeye ndiye aliyezusha upinzani mdogo kabisa.

Lakini hiyo haitoshi kabisa kuwa ni shuruti kwa wadhifa muhimu kama huo. Rais wa baraza la kudumu la Ulaya ni mtu ambaye atageukiwa kwa mashauriano na kutambuliwa na Rais Barack Obama wa Marekani au kiongozi wa China, Hu Jintao, kuwa ni Bwana Ulaya, mtu wa juu kabisa wa kuzungumza naye kutoka Ulaya. Jee kweli mtu anaweza kufikiria kwamba Van Rompuy atatoa mchango huo, atalijaza pengo hilo? Huenda yeye akawa mtu anayefaa katika kuowanisha mambo na mtu mwenye kutafuta muwafaka wa masuala yanayowatatiza watu, jambo ambalo pia, bila shaka, anatakiwa awe nalo. Lakini kama mtu muhimu wa kutoka Umoja wa Ulaya kuzungumza na Barack na Obama ni jambo ambalo ni shida kulifikiria.

Na mambo hayajakuwa bora pia kwa kumchagua Bibi Catherine Ashton kuwa mwakilishi mkuu wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya siasa za kigeni, ambao pia ni wadhifa wenye ushawishi mkubwa, tena kwa mtu ambaye ataonekana kuwa ni sura ya Ulaya duniani. Sio kwamba tunawapinga watu hao wawili, lakini bashasha ni kitu kingine.

Zikitaka zisitake, serekali za nchi za Umoja wa Ulaya zimechukuwa uamuzi wa mwelekeo. Bado Umoja wa Ulaya utaendelea kutoa mchango wa wastani katika uwanja wa siasa za kimataifa, mchango ambao ni chini ya uzito wake wa siasa zake za kiuchumi. Huenda hivyo ndivyo zilivotaka baadhi ya nchi. Kila wanapokuwa dhaifu wale wafanya kazi wanaotakiwa kuiwakilisha jumuiya nzima, ndipo wanavoweza zaidi wakuu wa serekali na nchi kuonesha misuli yao. lakini Ulaya inaweza tu kutetea maslahi yake ikiwa imeungana na kuwakilishwa kwa nguvu zaidi, tena kupitia wafanya kazi wake. Kinyume na hivyo ndivyo yaonesha itafanyika.

Huenda tunaweza kujipa faraja. Hii ni mara ya kwanza. Mara ya pili itakuwa mtu ameshajifunza.

Mwandishi: Christoph hasselbach/Miraji Othman/ZP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman