1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya, Uturuki zakubaliana kuhusu wakimbizi

Mohammed Khelef8 Machi 2016

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamemaliza mkutano wao wa kilele na Uturuki kwa makubaliano ya kihistoria katika kuukabili mzozo mkubwa kabisa wa wakimbizi tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

https://p.dw.com/p/1I8zd
Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Uturuki baada ya kumaliza mkutano wao wa kilele mjini Brussels.
Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Uturuki baada ya kumaliza mkutano wao wa kilele mjini Brussels.Picha: Reuters/Y. Herman

Siku mbili za mazungumzo ya kina, mijadala na hata upinzani kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels sasa zimetoka na matokeo ya kile kinachoweza kuitwa "nipa nikupe" baina ya Umoja huo na Uturuki.

Taarifa iliyotolewa leo baada ya mkutano huo, inasema pande hizo mbili zimekubaliana kulegezwa kwa masharti ya viza kwa Waturuki kuingia nchi za Umoja wa Ulaya na pia kwa kuharakishwa mazungumzo ya kujiunga na Umoja huo.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kampeni yake ya kuitaka Ulaya ifunguwe milango zaidi kwa wakimbizi, amewaambia waandishi wa habari kuwa Uturuki imejitahidi kufanya ya kutosha kwenye suala hili.

"Kwenye mpango huo tumeonesha wazi kwamba mengi yamekwishafanywa kuelekea ulinzi wa mipaka ya nje, Uturuki ikiwa imeshatekeleza hatua kadhaa, ikiwemo ya kuwapa wakimbizi vibali vya kufanya kazi. Uturuki pia imesisitiza kupatikana kwa euro bilioni 3 ambazo zilikubaliwa kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi ziweze pia kutumika kuanzisha miradi inayokwendana na azma hiyo, kama vile kufundisha kufundisha lugha ya Kiarabu," alisema Merkel mbele ya waandishi wa habari.

Ukweli kwamba Umoja wa Ulaya unatoa kiasi hicho cha fedha lilionekana kufahamika sivyo miongoni mwa vyombo vya habari barani Ulaya, na mapema leo takribani vyote viliripoti kuwa Uturuki itapewa pesa na Umoja wa Ulaya kama moja ya masharti ya makubaliano yaliyofikiwa. Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu, aliweka wazi kwamba nchi yake haijaomba pesa kutoka viongozi wa Umoja wa Ulaya na wala Umoja huo hautaipa pesa nchi yake.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu (katikati), akizungumza na Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu (katikati), akizungumza na Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.Picha: picture-alliance/dpa/C. Licoppe

"Euro hizi bilioni tatu zilitengwa na kukubaliwa kuwapa wakimbizi wa Syria. Ninasisitiza hilo. Euro hizo bilioni tatu haitapewa Uturuki, bali watapewa wakimbizi wa Syria. Hakuna hata euro moja itakayotumika kwa raia wa Uturuki," alisisita Davutoglu kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk.

Uturuki kuwachukuwa wakimbizi

Uturuki itawachukuwa pia wakimbizi ambao tayari wameshaingia kwenye ardhi za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini ambao bado hawajafika kituo cha mwisho cha safari zao.

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa, amesema hiyo ni hatua moja kubwa kuelekea kuukwamua mtanziko uliokaribia kuupasua Umoja wa Ulaya juu ya mzigo wa wakimbizi.

"Lengo ni kuzuia usafirishwaji usio wa kawaida wa wakimbizi kutoka Uturuki kwenda Ugiriki, na hatimaye imekubaliwa mambo matatu ya msingi: ulinzi wa mipakani, ushirikiano madhubuti na Uturuki na msaada unaofaa kwa Ugiriki," alisema Hollande.

Kufuatia makubaliano hayo, Tusk ametangaza kwamba siku za wahamiaji wa kiholela kuingia Ulaya zimemalizika.

Tusk amesema vipengele vya makubaliano kati ya pande hizo mbili vinamaanisha kuwa njia ya Balkan, ambayo ni mashuhuri kwa wakimbizi kumiminika barani Ulaya, sasa inafungwa rasmi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Oummlikheir Hamidou