1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waadhimisha miaka 60

Caro Robi
25 Machi 2017

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo Jumamosi mjini Rome, Italia kwa mkutano wa kilele wa kuadhimisha miaka sitini tangu kuundwa kwa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2ZwB2
Fahnen der  europäischen Mitgliedsstaaten
Picha: picture-alliance/dpa/K. J. Hildenbrand

Miaka sitini iliyopita, Uingereza haikudhuria mkutano mjini Rome ambako nchi sita jirani zilizokumbwa na vita zilianzisha kile sasa kinajulikana Umoja wa Ulaya. Leo Jumamosi, Uingereza kwa mara nyingine haitakuwa katika maadhimisho ya miaka sitini tangu kuasisiwa kwa Umoja wa Ulaya.

Mnamo tarehe 25 Machi 1957, nchi ambazo zilikuwa mahasimu Ufaransa na Ujerumani pamoja na Italia, Uholanzi, Ubelgiji na Luxembourg zilitia saini mkataba wa Roma. Leo ingekuwa mkutano wa kilele wa kawaida kwa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya kusheherekea miaka sitini ya Umoja huo, lakini maadhimisho hayo yanaghubikwa na kuondoka kusikotarajiwa kwa mmoja wa nchi wanachama- Uingereza.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May Jumatano wiki ijayo ataanza rasmi mchakato wa kujiondoa kwa nchi yake kutoka Umoja wa Ulaya. Uchumi wa nchi za Umoja wa Ulaya unakua japo kwa kasi tofauti baada ya mzozo wa kiuchumi uliozikumba katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na mzozo wa wakimbizi ambao ulizikumba nchi hizo unaonekana sasa kudhibitiwa.

Umoja wa Ulaya miaka 60 bila ya Uingereza

Lakini kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya almaarufu Brexit mchakato unaotarajiwa kukamilika Machi 2019, kumesababisha mashaka katika umoja huo ambao umejivunia miaka 60 ya umoja na amani na kustawi kwa pamoja.

Brexit-Hauptakteure - Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/M. Cardy

Kujiondoa kwa Uingereza kumewatia moyo wanasiasa wenye misimamo mikali ya kizalendo barani Ulaya kutaka nchi zao kuchukua mkondo wa Uingereza na pia kuzidisha tofauti miongoni mwa serikali za kitaifa na kupelekea waandaji wa maadhimisho hayo ya miaka 60 kutoandaa sherehe kubwa ya kusherehekea umoja wao.

Uingereza ilisusia kuasisiwa kwa mkataba wa Rome lakini ilibadili msimamo wake kuhusu soko la pamoja miaka mitatu baadaye. Hata hivyo ilibidi isubiri hadi mwaka 1973 kabla ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Mwezi Juni 2016, nchi hiyo ilipiga kura ya maoni kuamua iwapo isalie katika umoja huo au ijiondoe na hatimaye kura ya kujiondoa ilishinda.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewaambia viongozi wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya jana Ijumaa katika makao makuu ya Kanisa hilo ya Vatican kuwa umoja huo umepata mafanikio makubwa katika miaka 60 iliyopita lakini Ulaya inakabiliwa na kile alichokitaja 'ombwe la maadili'.

Amelaani kuongezeka kwa siasa kali za mrengo wa kulia za kizalendo zinazowabagua wahamiaji na itikadi kali ambazo amesema zinatishia kuwepo kwa Umoja wa Ulaya. Papa huyo ambaye si raia wa Ulaya amesema mwili ukipoteza dira na hauwezi tena kuangalia mbele unakumbwa na hali ya kudumaa na baadaye unakuwa katika hatari ya kufa iwapo hautakuwa na maono mapya.

Umoja wa Ulaya watakiwa kuwa na maadili

Papa Francis amewahimiza viongozi kuimarisha maadili na misingi ya Ulaya kwa kujituma zaidi na kuonyesha mshikamano zaidi.

Vatikan Papst
Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Papa FrancisPicha: picture-alliance/AP Photo/L'Osservatore Romano

Usalama umeimairishwa katika kasri la Campidoglio katikati mwa mji wa Rome ambako sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya Umoja wa Ulaya zinafanyika. Kiasi ya askari 3,000 wanashika doria katika mitaa ya Rome.

Polisi wakiwa katika hali ya tahadhari kuu baada ya shambulizi la kigaidi lililotokea London mji mkuu wa Uingereza.Takriban waandamanaji 30,000 wanatarajiwa kufanya maandamano manne tofauti ya kuunga na kuupinga umoja huo.

Uhamiaji, mzozo wa madeni unaoikumba kanda inayotumia sarafu ya euro, ugaidi na kuimarika kwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia za kizalendo umeuacha Umoja wa Ulaya uliobuniwa kutoka majivu ya vita vya pili vikuu vya dunia ukitafuta majibu mapya ya kukabiliana na changamoto unaoizikabili.

Viongozi wametia saini azimio la Rome linalotangaza kauli mbiu 'Ulaya ndiyo mustakabali wetu wa pamoja' baada ya mizozo ambayo imeutikisa misingi ya umoja huo. Lakini licha ya viongozi kutia saini azimio hilo, wamegawanyika pakubwa kuhusu njia ya kufuatwa kuhusu mustakabali wa siku za usoni wa Umoja huo.

Waziri mkuu wa Poland Beata Szydlo amekubali kutia saini azimio hilo katika dakika za mwisho akipinga vikali wazo la kuwepo na Ulaya yenye mifumo tofauti ya kujiendeleza kiuchumi unaopigiwa upatu na Ujerumani na Ufaransa zinazonuia kushirikiana zaidi zikiwa ndani ya Umoja wa Ulaya.

Poland inatiwa wasiwasi kuwa kama mojawapo ya nchi tisa zilizo nje ya kanda inayotumia sarafu ya euro, huenda ikaachwa nyuma iwapo nchi zinazotumia sarafu ya euro zitaruhusiwa kujiendeleza kivyao.

Ugiriki ambayo imekuwa ikipinga vikali sera za kukaza mkwiji ambazo zimepelekea nchi hiyo kupewa mikopo ya kuukwamua uchumi wake mara tatu inasisitiza azimio hilo la maadhimisho hayo ya miaka sitini yaangazie zaidi sera za kijamii.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Yusra Buwayhid