1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waidhinisha opereshini dhidi ya maharamia

Hamidou, Oumilkher10 Novemba 2008

Mawaziri wa ulinzi wapania kuona harakati za maharamia zinakoma katika bahari ya hindi

https://p.dw.com/p/Fqvn
Nembo ya NATO dhidi ya maharamia wa kisomaliPicha: AP/DW


Umoja wa Ulaya umeidhinisha hii leo opereshini za kijeshi baharini kupambana na maharamia katika fukwe za Somalia na katika Ghuba ya Aden.



Hizi ni opereshini za kwanza za  aina yake katika historia ya Umoja wa Ulaya.Opereshini "EUNAVFOR " kama zinavyoitwa zimeidhinishwa na mawaziri wa ulinzi kutoka nchi 12 za Umoja wa Ulaya,waliokutana mjini Brussels, na zinatazamiwa kuanza mapema mwezi ujao,katika mwambao wa pembe ya Afrika.


Kutokana na kuzidi hujuma za maharamia katika maeneo hayo,Umoja wa ulaya ulianzisha "tume ya ushirikiano" dhidi ya maharamia.Manuari mbili za kijeshi za Ufaransa na ndege ya doria ya Hispania zinasimamia opereshini za tume hiyo .

Japo kama kiongozi wa opereshini hiyo, anajulikana,nae ni naibu amiri jeshi wa kiengereza Philipp Jones,na Northwood,mji wa mwambao wa Uengereza ndio utakao kua makao makuu ya opereshini hizo -hata hivyo haijulikiani bado nchi ngapi zitashiriki.


Ujerumani,Ufaransa,Uengereza na Hispania zimeshaelezea utayarifu wao.Nchi nyenginezo ni pamoja na Uholanzi,Ubeligiji,Ureno,Ugiriki,Italy ,Luxembourg,Rumania,Slovakia na jamhuri ya Tcheki.


Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung anasema:


"La muhimu zaidi ni kukomesha uharamia,kurejesha hali ya usalama na kuhakikisha shughuli za kiibiashara zinaendelea ipasavyo."


Opereshini ya EUNAVFOR itakua na manuari zisizopungua sabaa ,tatu kati ya hizo ni za kivita pamoja na ndege za kupiga doria.


Marekani na washirika wake wengine wa magharibi wana manuari zao pia katika fukwe za Somalia ambako visa vya maharamia vinazidi kuongezeka.


Meli zisizopungua 18 zimeshambuliwa na maharamia wa kisomali katika bahari ya hindi na Ghuba ya Aden mnamo mwaka huu,visa ambavyo vimepindukia mara dufu visa kama hivyo vilivyoripotiwa  kipindi kizima cha mwaka jana.


Hata hivyo Yemen imeelezea wasi wasi wake hii leo kutokana na mpango  huo wa Umoja wa Ulaya wa kutuma manuari zake katika fukwe za Somalia na Ghuba ya Aden.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Yemen Abou Bakr Korbi amesema opereshini hizo zinaweza kutishia usalama wao na kufungua njia wakati huo huo ya kuigeuza bahari ya Sham kua ya kimataifa-"kama ilivyowahi wakati mmoja kupendekezwa na Israel na kukataliwa na waarabu."


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Yemen amesema nchi yake inapendelea  nchi za eneo hilo zidhamini usalama wa bahari ya Sham na bahari ya kiarabu katika mapambano dhidi ya maharamia.