1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa ulaya waitanabahisha jamhuri ya Tcheki

Oumilkher Hamidou7 Oktoba 2009

Waziri mkuu Jan Fischer ahakikisha nchi yake itaidhinisha mkataba wa Lisbon

https://p.dw.com/p/K1Jt
Rais wa jamhuri ya Tcheki Vaclav Klaus(mbele) akiongoza maandamano ya wapinzani wa mkataba wa LisbonPicha: AP

Umoja wa Ulaya umepania kuwatanabahisha viongozi wa jamhuri ya Tcheki, lakini bila ya kumuudhi rais Vaclav Klaus,watie saini haraka iwezekanavyo mkataba wa Lisbone.Hii leo viongozi wa Umoja wa Ulaya walikua na mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa jamhuri ya Tcheki Jan Fischer.

Baada ya mazungumzo yake pamoja na viongozi wa umoja wa ulaya,kuhusu umuhimu wa nchi yake kuidhinishwa mkataba wa Lisbonne ,waziri mkuu wa jamahuri ya Tcheki Jan Fischer amesema anaamini ni suala la wakati tuu hadi rais Vaclav Klaus atakapoamua kutia saini mkataba huo.

Jan Fischer aliyeshindwa kwenda Bruxelles kwasababu ya tatizo la ndege,alikua na mkutano kwa njia ya video pamoja na wakuu wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya,bunge la Ulaya na serikali ya Sweeden;mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulaya. Akizungumza na waandishi habari mwishoni mwa mkutano huo,waziri mkuu huyo wa jamhuri ya Tcheki,Jan Fischer amesema anaamini utaratibu wa kuidhinishwa mkataba wa Lisbonne utakamilika mhula wa mwenyekiti wa sasa utakapomalizika,mwishoni mwa mwaka huu.

"Nnadhani hakuna haja ya kuingiwa na wasi wasi.Katika jamhuri ya Tcheki,suala "sio ndio au la,bali lini mkataba wa Lisbonne utatiwa saini."Amesema waziri mkuu huyo akisisitiza bunge na baraza la Senet wameshaelezea uungaji mkono wao kwa mkataba huo.

"Mahakama ya katiba itakapopitisha uamuzi wake,rais hatokua tena na sababu ya kuchelewesha utaratibu wa kutia saini mkataba huo," amesema .

Mkataba wa Lisbonne utakaorahisisha utaratibu wa kupitisha maamuzi katika Umoja wa ulaya na kuimarisha nguvu za jumuia hiyo katika daraja ya kimataifa,umeidhinishwa hadi sasa na mataifa 24 kati ya 27 wanachama wa umoja wa ulaya.

Irland Referendum EU-Reformvertrag Feier
Wananchi walio wengi wa Ireland wanashangiria mkataba wa LisbonPicha: AP

Katika jamahuri ya Ireland wapiga kura wameunga mkono kwa wingi mkataba huo, kura ya maoni ilipoitishwa wiki iliyopita.Na rais wa Poland Lech Kaczynski ameahidi kuudhinisha mkataba huo mnamo siku zijazo.

Waziri mkuu wa Sweeden Frederik Reinfeld ,mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya,amesema anaamini mkataba wa Lisbonne utaidhinishwa.Hata hivyo amesema kuna haja ya watu kuwa na tahadhari.

"Tumeanza kuachana na mkataba wa Nice na kujivunia mkataba wa Lisbonne.Lakini kabla hatukupata uhakika wa lini utaanza kufanya kazi,hatutoanza kushauriana kuhusu wadhifa wa rais wa baraza la umoja wa ulaya na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje" amesema hayo waziri mkuu wa Sweeden Frederik Reinfeld,wakati wa mkutano na waandishi habari pamoja na spika wa bunge la Ulaya Jerzy Buzek na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya José Manuel Barroso.Jukumu letu ni kuhakikisha mkataba wa Lisbonne unaanza kufanya kazi hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu".Amesisitiza.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman