1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya sheria za kurudisha makwao wahamiaji wasio halali.

Mohamed Dahman5 Juni 2008

Mawazri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya sheria zenye utata zitakazotumiwa kwa pamoja na nchi zao juu ya kuwarudisha makwao wahamiaji wasio halali.

https://p.dw.com/p/EEOg
Wanaharakati wanaopinga kurudishwa watu makwao kutoka Ujerumani wakiwa na tambara lililoandikwa kwa lugha ya Kijerumani 'Mshikamano dhidi ya kurudishwa watu makwao'Picha: picture-alliance / dpa

Wahamiaji hao wasio halali wanaweza kupigwa marufuku kuingia Ulaya kwa miaka mitano iwapo watagoma kurudishwa makwao.

Sheria hizo mpya zilipitishwa na mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg hapo Alhamisi.

Taarifa kutoka kwa nchi inayoshikilia urais wa umoja huo Slovenia imesema urais wa umoja huo unataraji bunge la Umoja wa Ulaya kuunga mkono sheria hizo katika kikao chake cha mwezi wa Juni.

Makubaliano juu ya sheria hizo mpya yanatazamiwa kutiwa saini na bunge la Umoja wa Ulaya katika kikao chake mjini Strasbourg kati ya tarehe 16 na 19 mwezi wa Juni.

Sheria hizo mpya zitawalazimisha maafisa wa serikali katika mataifa ya Umoja wa Ulaya kuchaguwa kati ya kuwapa vibali vya ukaazi au vibali vya aina nyengine wahamiaji wasio halali kutoka nje ya umoja huo au kuwarudisha katika nchi walikozaliwa.

Sheria hizo zinaweka kikomo cha kuzuiliwa mahabusu wahamiaji wasio halali,zinaratibu urudishaji makwao kwa wahamiaji hao wasio halali na kuainisha taratibu ambapo kwayo mashirika yasio ya kiserikali yanaweza kuingia kwenye vituo vya mahabusu vya Umoja wa Ulaya hata hivyo sheria hizo haziwagusi watu wanaoomba hifadhi.

Sheria hizo zimepunguza hadi miezi sita kipindi ambacho kwayo wahamiaji wasio halali wanaweza kushikiliwa na serikali za mataifa wanachama.

Lakini muongozo wa sheria hizo umeshutumiwa na makundi yenye kutowa shinikizo kwa serikali kwa suala la haki za binaadamu kwa sababu ya kuruhusu muda wa mwisho wa kuwekwa mahabusu kuweza kuongezwa kwa miezi 12 zaidi katika baadhi ya kesi kwa mfano iwapo mhamiaji anagoma kutowa ushirikiano wake.

Hata hivyo mbunge wa chama cha SPD cha Ujerumani katika bunge la Umoja wa Ulaya ambaye pia ni wakili wa haki za binaadamu Wolfgang Kreissi- Dörfler amepokea vizuri marekebisho ya sheria hizo.

(O-Ton Dörfler)

Muhimu ni kwamba masharti kwa ajili ya binaadamu kulazimika kurudishwa makwao kama sheria inavyosema yameboreshwa kwamba watoto na familia hawatolazimika kwenda gerezani kwamba haiwezekani tena kwa watu inaobidi warudishwe makwao ambao hawakuwahi kufanya makosa ya jinai kuwekwa pamoja gerezani na watu waliofanya makosa na kuhukumiwa.

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zimekataa wito wa kutowa msaada wa kisheria bila ya malipo kwa wahamiaji wote na badala yake zimekubaliana na muafaka kwamba kipengele cha aina hiyo kiambatane na sheria za taifa zilioko hivi sasa.

Sheria hizo mpya kwa kiasi kikubwa zitawalenga wale ambao wananchi wa Ulaya hawawatuhumu kabisa kama wamevunja sheria nao ni wale walioendelea kubakia katika nchi baada ya kumalizika wa muda wa viza zao ambao wanakadiriwa kufikia takriban milioni 12 ambalo ni fungu kubwa kabisa la wahamiaji wasio halali katika nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya.

Wahamiaji hao wasio halali mara nyingi hutokea Ufilipino,raia kutoka China na Ukraine au Amerika ya Latin na mataifa ya Afrika hata hivyo wanaweza kuwemo pia raia wa Marekani,Japani na kwengineko.

Wahamiaji hao wasio halali hingia kwa kutumia viza ya utalii kabla ya kujumika vizuri katika jamii na kufanya kazi katika masoko ya magendo yumkini wakawa wasafishaji,waangalizi wa watoto katika familia au wafanyakazi ngumu katika viwanda au pengine wafanyakazi wa mikahawa.

Sheria hizo mpya hazitowalenga wale wanaotafuta hifadhi ambao huelekea fukwe za Italia, Ufaransa, Malta au Uhispania baada ya safari zao za hatari kutoka Afrika Kaskazini.

Chini ya sheria hizo mpya mhamiaji asie halali atakuwa ana mawili ya kuchaguwa : arudi nyumbani au arudishwe kwa nguvu.

Mjadala juu ya Mungozo wa Sheria hizo mpya umekuja katika kipindi nyeti kwa Ulaya ambapo baadhi ya serikali zikitaka kupambana vikali na wimbi la wahamiaji linaloonekana kutozuilika kutoka Afrika na Asia.