1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wamuandalia vikwazo vingine Assad

Admin.WagnerD20 Aprili 2012

Umoja wa Ulaya umesema umetayarisha vikwazo vipya dhidi ya utawala wa rais Assad, vinavyolenga kuudhoofisha zaidi usiendelee na ukandamizaji.

https://p.dw.com/p/14iVG
Bashar Assad
Bashar AssadPicha: AP

Vikwazo hivi vipya vitajulisha kupiga marufuku uuzaji wa vitu vya anasa na bidhaa nyingine zinazoweza kutumiwa na utawala huo kundeleza ukandamizaji.

Mwanadiplomasia mmoja kutoka Umoja wa Ulaya ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema vikwazo vipya vimekwisha tayarishwa na utekelezwaji wake unaweza kuamuliwa wakati wa Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo, unaofanyika mjini Luxemburg siku ya Jumatatu kulingana na hali itakavyokuwa.

Mwezi uliyopita, Umoja wa Ulaya uliwawekea vikwazo vya kusafiri na kufanya manunuzi katika kanda hiyo, watu wa karibu wa rais Assad, akiwemo mkewe, mama na dada yake. Vikwazo hivi pia vilihusisha kampuni kampuni mbili za mafuta na kufanya idadi ya waliowekewa vikwazo kufikia watu 126 na kampuni 14.

Mandamano dhidi ya serikali ya rais Assad
Mandamano dhidi ya serikali ya rais AssadPicha: Reuters

Mlipuko waua wanajeshi 10
Wakati huo huo, Televisheni ya Taifa ya Syria imeripoti kuwa mlipuko kubwa umeua maafisa 10 wa jeshi katika eneo la Quneitra.

Imesema magaidi waliyo na silaha wamelipua bomu lililokuwa na uzito wa kilo 100 katika mji wa Sahm al Jolan ulioko katika jimbo la Quneitra, karibu na mpaka wa Israel. Tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpnago wa amani tarehe 12 Aprili, wati 120 wameripotiwa kuuwa.

Hayo yametokea wakati wapinzani wanafanya mandamano ya baada ya swala ya Ijumaa yanayolenga kupima utayari wa utawala wa rais Assad kuheshimu mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa, ambao Katibu Mkuu Ban Ki-Moon tayari amesha sema kuwa utawala huo umeshindwa kuuheshimu.

Maelfu washiriki mandamano
Mandamano ya siku ya Ijumaa yalihudhuriwa na maelfu ya wananchi katika miji mbalimbali waliyokuwa wakirudia rudia maneno ya "Tutashinda na Assad ataondoka." Picha za video zilizowekwa katika mtandao zimeonyesha maelfu wakishiriki mandamano katika mji wa Hassaka unaokaliwa na Wakurd wengi.

Wengine wameshuhudiwa katika mkoa wa Daraa ambao ni chimbuko la harakati za uasi dhidi ya serikali ya Assad, na pia katika mji mkuu Damascus. Wanaharakati wameripoti kuwepo kwa wanajeshi wengi katika maeneo mbalimbali nchini humo licha ya serikali kuahidi kuwarudisha wanajeshi hao kambini.

Ufaransa yaanda muswada mpya
Tayari Ufaransa imeshaanza kuandaa rasimu ya azimio la kupeleka katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kuongeza idadi ya waangalizi hadi kufikia 500 kwenda nchini Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Alain Juppe amesema waangalizi hao watahitaji kuwezeshwa vizuri ili kuwahakikishia wananchi wa Syria uhuru wa kuandamana.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa
Walinda amani wa Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa

"Kwentu jambo la muhimu zaidi ni utekelezaji wa Mpango wa Annan wa amani. Ndiyo nafasi yetu ya mwisho ya kurejesha amani, nafasi ya mwisho ya kuepusha kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe," alisema Juppe.

Katibu Mkuu ban Ki-Moon, amesema kuna ushahidi kwamba serikali ilikuwa inafanya ukandamizaji dhidi ya raia licha ya kukubali kusitisha vurugu. Amesema taarifa zinaonyesha vurugu zimeongezeka katika siku chache zilizopita zikihusisha mashambulizi dhidi ya raia, unyanyasaji unaofanywa na vikosi vya serikali na uvamizi wa makundi yenye silaha.

Siku ya Alhamis, Syria na Umoja wa Mataifa walisaini makubaliano yanayowaruhusu wangalizi wa Umoja huo kuingia nchini humo na kufuatilia utekelezaji wa mpango wa amani.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman