1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wapiga vita picha za watoto walio uchi

Charo Josephat/ Hasselbach25 Machi 2009

Nchi wanachama kushirikiana kupambana na picha za ponografia za watoto

https://p.dw.com/p/HJbK
Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na sheria, uhuru na usalama, Jacques BarrotPicha: picture alliance / Photoshot

Umoja wa Ulaya unaimarisha vita dhidi ya ponografia kwenye mtandao wa mawasiliano wa intaneti. Umoja huo unapanga kuzuia ununuzi wa picha za watoto wakiwa uchi zinazotia ashiki kutumia kadi za benki.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maswala ya ndani ya umoja huo, Jacques Barrot, ni mtu makini anapozungumza lakini linapokuja swala la ponografia ya watoto huzungumza kwa ukali kama alivyofanya mwezi uliopita wakati alipokuwa akilihutubia bunge la Ulaya.

"Tunafahamu mtu anapochukua hatua za haraka na kutoa onyo, anaweza kuzuia kupotea kwa watoto. Hili ningependa kulisisitiza katika bunge la Ulaya linapokuja swala hili la watoto wanapopotea hususan kwa lengo la kutumiwa kwa picha za uchi na kimapenzi."

Ukweli ni kwamba watoto hawapotei, hasa kupitia kutekwa nyara. Kwa sababu mara kwa mara ni jamaa na hata wazazi wanaopiga picha za ponografia na watoto wao wenyewe na kisha kuzituma kwenye mtanda wa intaneti. Bunge la Ulaya inaliona tatizo hili katika malezi. Kupitia mazungumzo kwenye kompyuta kwa njia ya mtandao, watu wazima huanza mawasiliano na watu waliotoa umri ambao sio, na majina ya uongo, na hivyo kuanza kuwasiliana na watoto kwa lengo la kujifurahisha kimapenzi. Roberto Angelilli ni muandaaji wa ripoti kuhusu ponografia ya watoto katika bunge la Ulaya.

"Kila nchi mwanachama inatakiwa kuwaq na sheria za kuadhibu tabia ya kubadili saikolojia ya mtu kupitia mtandao wa mawasiliano wa intaneti, kwa lengo la hujuma za kimapenzi."

Nchini Ujerumani hali tayari iko namna hii. Bunge la Ulaya linataka kuongeza vikwazo katika nchi wanachama wake dhidi ya picha za ponografia ya watoto na matayarisho ya picha hizo. Shida kubwa iliyopo ni kwamba kampuni zinatuma picha za watoto walio uchi kwenye mtandao wa intaneti hutokea nje ya Umoja wa Ulaya na hubadili mara kwa mara makao ya shughuli zao. Kwa sababu hiyo, Umoja wa Ulaya hautaki tu kushirikiana na maafisa wa sheria wa nchi wanachama, bali pia kuboresha ushirikiano wake na nchi zinazoendelea. Mwanasiasa wa Ujerumani Wolfgang Kreissl-Döfler anasisitiza pia kuhifadhi data kutoka kwa wanaotuma na kutumia picha za ponografia. Je hatua hiyo haifungui mlango kwa matumizi mabaya ya data?

Bwana Kreissl-Dörfler anasema, "La muhimu ni iamuliwe wazi ni nani ana mamlaka, ni kitu gani kitakachofanywa na vipi data zitakavyofutwa tena. Hayo naweza kuyashughulikia."

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inataka pia kuzuia ununuzi wa picha za uchi za watoto kutumia kadi ya mkopo na kushirikiana na kampuni zinazomiliki kadi hizo. Juu ya hayo kiwango cha yuro nusu milioni kimewekwa tayari kwa mtandao unaotakiwa kusaidia kuwafichua watumaji na watumiaji wa picha watoto walio uchi kwenye mtandao.

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekubaliana kwamba zinatakiwa kufanya juhudi zaidi kupambana na ponografia ya watoto. Bila shaka swala la sheria na maendeleo ya kiufundi ya mtandao wa mawasiliano wa intaneti kunavifanya vita hivi kuwa kibarua kigumu.