1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wataka Mursi aachiwe huru

18 Julai 2013

Waandamanaji wanaomuunga na wapinzani wa Mursi wameandamana kote Misri wakati mkuu wa sera za nje akitowa mwito wa kuachiwa huru kiongozi huyo anayezuiliwa na jeshi.

https://p.dw.com/p/19A7e
Rais wa mpito Adli Mansour na makamu wake Mohammed Elbaradei wakikutana na Catherine Ashton Kairo.
Rais wa mpito Adli Mansour na makamu wake Mohammed Elbaradei wakikutana na Catherine Ashton Kairo.Picha: picture-alliance/dpa

Maandamano yalianza jumatano usiku baada ya mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton kutaka rais Mursi aachiwe huru.Mwito huo umetolewa baada ya Ashton kukutana na rais wa mpito Adly Mansour pamoja na makamu wake anayehusika na masuala ya uhusiano wa Kimataifa Mohammed ElBaradei.

Mwito wa Ashton

Ashton amesema anaamini Mursi anastahili kuachiwa huru,ingawa hakuweza kukutana nae amehakikishiwa rais huyo anayeshikiliwa mahala kusiko julikana yuko salama.Ashton amekutana lakini na viongozi wa chama cha Mursi cha udugu wa kiislamu akiwemo waziri mkuu Hisham Kandil na kuvishawishi vyama vyote kujiunga katika mchakato wa kutafuta maridhiano.Ripoti lakini zinasema hakujakuweko miito ya kutaka Mursi arejeshwe madarakani.

Wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wakifyatuliwa vitowa machozi na polisi
Wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wakifyatuliwa vitowa machozi na polisiPicha: Reuters

Mkuu wa sera za nje ameliambia shirika la habari la Uingereza BBC kwamba amejadiliana na serikali ya mpito juu ya uwezekano wa Umoja wa Ulaya kusaidia katika shughuli za chaguzi zijazo ikiwemo usaidizi wa kusimamia shughuli hizo.Hata hivyo mwito wa kulitaka kundi la Udugu wa Kiislamu lishiriki mazungumzo ya maridhiano umetolewa wakati ambapo kuna maandamano ya wafuasi na wapinzani wa Mursi mjini Cairo ambapo yaliendelea hadi mapema asubuhi ya leo (Alhamisi).

Mapema jana Jumatano msemaji wa chama cha Udugu wa kiislamu Gehad El-Hadad alisema katika ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Umoja wa Ulaya umelaani waziwazi mapinduzi ya kijeshi pamoja na nchi zilizotangaza kuyatambuwa mapinduzi hayo au serikali iliyopo.

Umwagikaji wa damu

Wakati huohuo umwagikaji wa damu unashuhudiwa nchini humo,ambapo katika eneo la kaskazini mwa Sinai wanamgambo wamewauwa polisi watatu usiku wa kuamkiaAlhamisi (18.07.2013) katika matukio tofauti.

Wanajeshi wa Misri wakiwa mji wa El Arish,katika rasi ya Sinai
Wanajeshi wa Misri wakiwa mji wa El Arish,SinaiPicha: picture alliance/dpa

Duru za hospitali na zile za usalama zimearifu kwamba watu watatu waliokuwa na bunduki walikivamia kituo cha polisi katika mji wa Sheikh Zuweid na kuwajeruhi maafisa watatu katika mapambano ya risasi kabla ya kukimbia.Polisi mwingine aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa na silaha nje ya nyumba yake katika mji wa El-Arish katika kile kinachotajwa kuwa matukio ya karibuni kabisa ya umwagikaji damu yaliyopamba moto katzika rasi hiyo ya Sinai.

Wadadisi wa mambo wanasema ghasia na mauaji katika eneo hilo la Sinai zinasababishwa na makundi ya itikadi kali za kiislamu yanayotaka kutumia fursa hii ya mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini Misri baada ya Mursi kutimuliwa madarakani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman