1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watunukiwa Nishani ya Amani ya Nobel

12 Oktoba 2012

Umoja wa Ulaya umetunukiwa tuzo ya mwaka huu ya amani ya Nobel baada ya Kamati ya Nobel nchini Norway kuridhika kwamba Umoja huo umekuwa katika mstari wa mbele kupigania na kueneza demokrasia Ulaya na duniani kwa jumla.

https://p.dw.com/p/16OmI
Alama ya Nishani ya Amani ya Nobel.
Alama ya Nishani ya Amani ya Nobel.Picha: Reuters

Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Nobel, Thorbjorn Jagland amesema cha msingi kilichowafikisha katika uamuzi wa pamoja wa kutoa tuzo hiyo kwa Umoja wa Ulaya ni juhudi za Umoja huo za kuleta amani na maridhiano pamoja na demokrasia katika Umoja huo baada ya vita vya pili vya dunia

Tuzo hiyo inaonekana kama hatua ya kuupa nguvu na mori muungano huo wakati ukiwa katika mapambano ya kuutatua mgogoro wake wa madeni. Kamati hiyo imezipongeza nchi wanachama 27 kwa kuujenga upya umoja wao baada ya Vita vya Pili vya Dunia pamoja na kazi iliyoifanya katika kueneza utulivu katika nchi zilizokuwa za Kikomunisti baada ya kuangushwa ukuta wa Berlin mwaka 1989.

Tuzo ya Amani ya Nobel inayoambatana na zawadi ya fedha dola milioni 1.2 itakabidhiwa rasmi kwa Umoja huo katika sherehe itakayofanyika mjini Oslo, Norway, hapo tarehe 10 Disemba.

Bunge la Ulaya laisifu heshima ya Nobel

Spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz amelipokea kwa furaha tangazo la ushindi huo wa tuzo ya Nobel kupitia taarifa aliyoitoa hivi punde kupitia mtandao wa Twitter, akisema hatua ya kamati ya Nobel kutambua maridhiano ya baada ya vita vya pili vya dunia barani Ulaya ni jambo la kutia moyo.

Bunge la Umoja wa Ulaya.
Bunge la Umoja wa Ulaya.Picha: Reuters

Amesema Umoja wa Ulaya unahusu Maridhiano, Umoja wa Ulaya ni mradi wa kipekee uliovitenga vita na kuchukua njia ya amani kwa kuleta mshikamano kupambana na chuki.

Umoja huo uliasisiwa mwaka 1957 kupitia mkataba wa Roma ukianzia na wanachama sita waliokuwa na lengo la kutafuta ushirikiano wa kiuchumi na kufikia sasa ni nchi 27 zinazounda Umoja huo zikiwemo nchi za Ulaya Mashariki zilizojiunga baada ya Vita Baridi.

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umekumbwa na mgogoro huku kukiweko na hali ngumu kwenye eneo lake la Sarafu ya Euro inayotumiwa na nchi 17 za Umoja huo.

Kutoka na hali hiyo tuzo ya amani ya Nobel imekuja kwa mshangao kwa wengi hasa kutokana na mvutano huo wa sarafu ya Euro. Wengi wa Wanorway wanaupinga Umoja wa Ulaya kwa kuuona kama ni kitisho kwa uhuru wa nchi zinazouunda.

Itakumbukwa kwamba Norway kitovu cha tuzo ya Nobel, imepiga kura mara mbili za kukataa kujiunga na Umoja huo mwaka 1972 na mwaka 1994.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef