1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wazidisha vikwazo dhidi ya Syria

15 Oktoba 2012

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wametangaza vikwazo vipya dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad wa Syria, kuzitaifisha mali zake na kuwawekea vikwazo vya kusafiri Wasyria 28.

https://p.dw.com/p/16Q6X
Waziri wa Mambo wa Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kulia) na mwenzake wa Sweden, Carl Bildt.
Waziri wa Mambo wa Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kulia) na mwenzake wa Sweden, Carl Bildt.Picha: AP

Mkutano wa leo ambao ni wa 19 kuhusu vikwazo dhidi ya Syria tangu kuanza kwa mzozo nchini humo mwezi Machi, mwaka uliopita, unafikisha idadi ya watu 181 na kampuni 54 ambazo zimeorodheshwa na Umoja wa UIaya kwa ajili ya kuwekewa vikwazo.

Vikwazo hivyo vinawalenga watu waliohusika na unyanyasaji dhidi ya waandamanaji na vyombo vilivyoshiriki katika kusambaza vifaa vilivyotumika kwa ajili ya kuikandamiza serikali. Vikwazo hivyo vinaambatana na kuwazuia wakaaazi wa Umoja wa Ulaya kununua, kusafirisha au kusaidia kwa namna yoyote ile makampuni ya Syria ambayo yanafanya biashara ya silaha.

Aidha, mawaziri hao wanafikiria kuiwekea Iran vikwazo vipya saa chache baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia kuhusu sera za kigeni. Urusi imeunganisha nguvu zake na China katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala wa Syria.

Brahimi ataka Iran kusaidia amani ya Syria

Wakati huo huo, mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Lakdhar Brahimi, ameitaka Iran kusaidia katika kupatikana kwa amani ya Syria, wakati wa mapumziko ya siku nne ya Waislamu ya sikukuu ya Eid al-Adha, yanayotarajia kuanza juma lijalo. Brahimi amesema kuwa hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria inazidi kuwa mbaya. Amesisitiza umuhimu wa haraka wa kuzuia umwagikaji wa damu.

Waziri wa Mambo wa Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kulia) na mkuu wa sera za nje wa Ulaya, Catherine Ashton.
Waziri wa Mambo wa Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kulia) na mkuu wa sera za nje wa Ulaya, Catherine Ashton.Picha: picture alliance/ZUMA Press

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa, ameyatoa matamshi hayo leo mwishoni mwa ziara yake nchini Iran ambako alikutana na Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran, mshirika mkubwa wa Rais Assad. Brahimi anazuru eneo hilo kwa mazungumzo ya kutafuta njia ya kumaliza mzozo wa Syria. Hata hivyo, wito wa kumalizika kwa ghasia nchini Syria ambazo zimesababisha watu 33,000 kuuawa, umekuwa ukipuuzwa.

Wiki iliyopita, Brahimi alizuru Saudi Arabia na uturuki, mataifa mawili yenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Sunni ambayo yamekuwa yakiwaunga mkono wapinzani wa Syria. Aidha, alirudia wito uliotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon wa kumalizwa kwa mzozo nchini Syria na kuzuia upelekwaji wa silaha kwa pande zote zinazohasimiana.

Jana Uturuki ilitangaza kuzipiga marufuku ndege za abiria za Syria kuruka katika anga yake, uamuzi ambao pia umechukuliwa na Syria, wakati mvutano kati ya mataifa hayo mawili ukizidi kuwa mbaya, kutokana na wiki iliyopita Uturuki kuilazimisha ndege ya abiria ya Syria kutua Ankara, kwa madai kuwa ilikuwa zana za kijeshi.

Ama kwa upande mwingine idadi ya wakimbizi wa Syria wanaoishi kwenye kambi za wakimbizi nchini Uturuki, imefikia 100,000. Taarifa hiyo imetolewa leo na Shirika linalosimamia maafa la Uturuki-AFAD.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE/AFPE/APE/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman