1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umuhimu wa Kilimo na shughuli za mabwana shamba Afrika

Mohamed Dahman28 Aprili 2008

Kilimo barani Afrika kinakabiliwa na changamoto kubwa hususan wakati huu.

https://p.dw.com/p/DpjH
Msafara wa msaada wa chakula nchini SomaliaPicha: AP

Wakati huu ambapo kuna wasi wasi mkubwa wa kimataifa kuhusu mustakbali wa upatikanaji wa chakula duniani haya ni matamshi yanayofaa kutafakariwa : ' Nafundisha watoto wa chuo kikuu kilimo na shughuli za mabwana shamba lakini wengi wao hupendelea kujifunza kazi nyengine hususan fani ya teknolojia ya mawasiliano ya habari kwa sababu kilimo ni kwa ajili ya watu wasiokwenda shule.

Washington Ochola mhadhiri mwandamizi wa kilimo endelevu na maendeleo vijijini katika chuo Kikuu cha Egerton karibu na mji mkuu wa Kenya Nairobi ametowa matamshi hayo hivi karibuni katika mji mkuu huo wa Kenya wakati wa uzinduzi wa utafiti wa Tathmini ya Kimataifa ya Sayansi ya Kilimo na Teknolojia kwa ajili ya Maendeleo.Juhudi za miaka mitatu zimekusanya maoni ya wahusika wote katika kilimo kwa nia ya kuifanya sekta hiyo kuwa na ufanisi zaidi na endelevu.

Hata hivyo mbali ya kuwa kimbilio kwa wale ambao hawakupata elimu rasmi shughuli za mabwana shamba wa kilimo zinahitaji utaalamu mkubwa zaidi kwa wale wanaozitenda kutokana na wakulima kukabiliwa na matatizo ambayo katika kipindi cha kizazi kimoja kilichopita yalikuwa hayakufikiriwa kabisa.Mfano shinikizo la kufanya kazi katika masoko ya utandawazi duniani au kuzalisha mazao wakati virusi vya HIV na UKIMWI vikiangamiza nguvu kazi vijijini.Mabwana shamba imekuwa ni desturi kutumika kama daraja kati ya watafiti wanaobuni teknolojia mpya na wakulima wanaotekeleza teknolojia hizo kwa vitendo.

Vipi serikali nchini Kenya na kwengineko barani Afrika zitakabiliana na changamoto ya kutowa mabwana shamba wenye ujuzi mahiri na kuwawezesha wale ambao tayari wako kazini kutenda kazi zao kwa ufanisi zaidi kutatimiza dhima muhimu katika kuyakinisha iwapo kilimo kinatimiliza uwezo wake barani kote Afrika.Pia kutahitaji kuinuwa hadhi ya wafanyakazi hao kupindukia ile ya waajiriwa wa teknolojia ya habari na mawasiliano na hata kuongeza bajeti ya shughuli za mabwana shamba huenda likawa ni jambo linalobidi kufanywa.

Mabwana shamba wapo lakini hakuna vifaa vya kuwawezesha kutowa huduma zao kwa mkulima.Hivyo ndivyo anavyosema Daniel Otunge wa shirika lisilo la serikali lenye makao yake mjini Nairobi la Huduma ya Kimataifa kwa Matumizi ya Teknolojia ya Kilimo ambalo linajihusisha na upandikizaji wa mbegu ya ndizi na miti ya mikaratusi.

Anasema bila ya pikipiki bwana shamba hawezi kuwafikia wakulima ambao ni muhimu.

Kwa upande wake Ochola ambaye pia amechangia kuandika tathmini hiyo ya kilimo kusini mwa jangwa la Sahara anasema kutokuwepo kwa mtizamo wa pamoja kuwaelekeza wakulima kunapelekea kujirudia au mkorogo wa fikra kunakowachanganya wakulima.

Shughuli za mabwana shamba zimeonekana kuwa na manufaa zaidi kwa mashamba makubwa ya mazao kuliko kwa shughuli ndogo ndogo za aina mbali mbali za kilimo.

Mabwana shamba wanaodhaminiwa na wafadhili huweka ajenda zao ambapo mara nyingi zinakuwa dhidi ya matarajio ya wakulima.

Asilimia 83 ya mabwana shamba ni wanaume ambao yumkini wakapigwa marufuku kuwasiliana na wakulima wa kike kutokana na vikwazo vya kitamaduni licha ya kwamba wanawake wanafanya asilimia 70 ya wafanyakazi wa mashambani kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.

Inapendekezwa kwamba viwango vya elimu kwa wakulima wenyewe viboreshwe ili kuweza kuwasiliana vizuri zaidi na mabwana shamba venginevyo inakuwa vigumu kwao kurahisisha tafiti za kisayansi na kufuata maelekezo.

Ingawa kilimo kinashika nafasi ya tatu ya pato la jumla la ndani ya nchi kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika bado asilimia 30 ya watu wake wanakabiliwa na njaa.