Umwagaji damu usitishwe Syria
21 Januari 2012Licha ya tume ya umoja huo kukosolewa vikali, naibu mkuu wa operesheni za tume hiyo ya waangalizi, Ali Jarush amewaambia waandishi habari kuwa muda wa tume hiyo, huenda ukarefushwa kwa mwezi mmoja. Wakati huo huo, mkuu wa tume ya waangalizi, Jenerali Mohammed Ahmed Mustafa al-Dabi kutoka Sudan, anajiandaa kuwasilisha ripoti ya tume hiiyo kwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu, wanaokutana mjini Cairo siku ya jumapili, kujadili hatua inayofaa kuchukuliwa.
Lakini shirika linalotetea haki za binadamu "Human Rights Watch" linasema, kuwepo kwa tume hiyo ya Umoja wa nchi za Kiarabu huko Syria, wala haikusaidia kukomesha ukandamizaji unaofanywa na serikali ya nchi hiyo. Wanaharakati wanasema, tangu tume hiyo ya waangalizi ilipokwenda Syria Desemba 26, raia 506 wameuawa na wengine 490 wametiwa mbaroni. Sasa, Umoja wa Nchi za Kiarabu unahimizwa na shirika la "Human Rights Watch" kutamka hadharani kuwa Syria haikuheshimu mpango wa umoja huo.
Kwa hivyo, umoja huo sasa ndio uanze kushirikiana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuishinikiza serikali ya Syria na matumizi ya nguvu yasite. Mkuu wa Baraza la kitaifa la Syria (SNC), linalojumuisha makundi ya upinzani, Burhan Ghaliun amekwenda Cairo nchini Misri, kuwashawishi mawaziri wa nchi za Kiarabu kuiwasilisha ripoti ya tume ya waangalizi katika Baraza la Usalama ili hatua kali ipate kuchukuliwa. Wakati huo huo, shirika rasmi la habari la Misri, MENA limeripoti kuwa Ahmed el-Tayyeb, Imam mkuu wa Al-Azhar - kituo kikuu cha masomo ya Kiislamu mjini Cairo, amewahimiza viongozi wa Kiarabu kuchukua hatua zinazohitajika kusitisha umwagaji damu nchini Syria.
Kwa upande mwingine, waandamanaji wa Kisyria walioghadhibika, walikusanyika nje ya ubalozi wa Urusi mjini Cairo kutoa dukuduku lao kuhusu msimamo wa nchi hiyo kuiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria. Urusi na China zenye kura turufu katika Baraza la Usalama, zilipinga azimio lililopendekeza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya Syria. Mkwamo huo katika Baraza la Usalama humaanisha kuwa sasa viongozi wa Kiarabu ndio wanazidi kushinikizwa kutafuta suluhisho la mzozo wa Syria. Umoja wa Mataifa unatathmini kuwa zaidi ya watu 5,400 wameuawa katika ukandamizaji ulioanza mwezi Machi nchini Syria.
Mwandishi: Martin, Prema/afpe
Mhariri: Alakonya, Bruce