Umwagaji damu waendelea Syria
19 Novemba 2011Siku ya Ijumaa raia 12 waliuawa na vikosi vya usalama vya Syria. Watoto 2 ni miongoni mwa wahanga hao.Mauaji hayo yametokea wakati Uturuki na Marekani zikionya juu ya hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuibuka nchini Syria na huku maelfu ya watu wakiandamana barabarani bila ya kuvijali vikosi vya usalama vilivyosambazwa kwa wingi na kutoa mito ya kuwafukuza mabalozi wa Syria.
Uturuki imetahadharisha juu ya uwezekano wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokea wakati idadi ya wanajeshi wanaouawa na wenzao walioasi ikiongezeka. Onyo hilo pia limetolewa na wachambuzi wanaoyafuatiliza matukio ya nchini Syria inayozidi kutengwa kimataifa. Umoja wa Nchi za Kiarabu umeitaka Syria isitishe umwagaji damu wa waandamanaji, ifikapo usiku wa manane wa Jumapili ama sivyo itakabiliwa na hatari ya kuwekewa vikwazo. Uanachama wake katika Umoja wa Nchi za Kiarabu wenye mataifa 22 umesitishwa kwa muda.
Kwa upande mwingine, Iran imesema, hatua hiyo ni "kosa la kihistoria" na kwamba hatua hiyo ndio itakayosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kwa tathmini ya Umoja wa Mataifa, hatua za ukandamizaji zinazochukuliwa na serikali ya Syria kuyazima maandamano yaliyoibuka katikati ya mwezi Machi, zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,500.
Hapo mwanzoni, waandamanaji walimiminika barabarani kudai demokrasia katika nchi hiyo ya kiarabu inayotawalwa kwa mabavu, lakini sasa watu hao wanataka kuitimua madarakani serikali ya Rais Assad na wanaungwa mkono na wengi katika ulimwengu wa magharibi.
Mwandishi,Martin,Prema/afpe
Mhariri: Sekione Kitojo