1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Hakuna mahali palipo salama huko Gaza

26 Oktoba 2023

Umoja wa Mataifa umetoa onyo kali leo Alhamisi kwamba hakuna mahali palipo salama huko Gaza wakati mashambulizi ya anga ya Israel yakiendelea katika dhamira ya kuandaa mashambulizi mengine ya ardhini.

https://p.dw.com/p/4Y3BV
Gazastreifen | Rauchsäulen nach Raketeneinschlägen
Moshi mkubwa ukidhihirika huko Gaza baada ya mashambulizi ya anga ya Israel:23.10.2023Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Wakati Israel ikilipiza kisasi baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7 kwa mashambulizi ya karibu kila sehemu ya eneo la Palestina, watu wameachwa bila chochote ila chaguo lisilo na mustakabali wowote. Hayo ameyasema Lynne Hastings, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, na kusisitiza kuwa hakuna mahali salama huko Gaza.

Soma pia: UNRWA: Bidhaa ya mafuta yahitajika haraka Gaza

Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake na vifaru viliingia kwa muda mfupi kaskazini mwa Gaza usiku wa kuamkia leo na kuyashambulia maeneo kadhaa ya wanamgambo wa Hamas. Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Daniel Hagari amesema:

"Vikosi vyetu vimewaua magaidi na kuharibu miundombinu ya Hamas katika ukanda huo. Uvamizi huu ni sehemu ya maandalizi yetu kwa hatua zinazofuata za vita. "

Mashambulizi ya anga ya Israel yaliyodumu kwa zaidi ya wiki mbili, yameharibu sehemu za Ukanda wa Gaza huku hospitali za eneo hilo zikikabiliwa na uhaba wa vifaa vya matibabu kwa raia waliojeruhiwa.

Wito wa usitishwaji mapigano

Belgien, Brüssel | EU Pressekonferenz mit Charles Michel und Ursula von der Leyen
Viongozi wa Umoja wa Ulaya: Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya: Ursula von der Leyen (kwenye Runinga) na Charles Michel Rais wa Baraza la Ulaya wakizungumzia mzozo wa Mashariki ya Kati 17.10.2023Picha: Johanna Geron/REUTERS

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa hii leo kutoa wito wa usitishwaji mapigano na kuanzishwa kwa "ukanda salama" kwa ajili ya sababu za kibinadamu ili kuwezesha uwasilishwaji wa misaada muhimu inayohitajika haraka huko Gaza.

Hayo ni kulingana na rasimu ya mwisho inayotazamiwa kuafikiwa katika mkutano wa kilele mjini Brussels leo Alhamisi ambayo imesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya utafanya kazi kwa karibu na washirika wake eneo hilo ili kuwalinda raia, kutoa msaada na kuwezesha upatikanaji wa chakula, maji, huduma za matibabu, mafuta na malazi, na zaidi sana kuhakikisha kwamba msaada kama huo hautumiwi vibaya na mashirika ya kigaidi.

Israel imesema inajiandaa na mashambulizi ya ardhini ikilenga kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Hamas

Kwa upande mwingine, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis na kumueleza kuwa mashambulizi huko Gaza yamekuwa ni mauji ya jumla na kwamba ukimya wa jumuiya ya kimataifa unatia aibu. Aidha Erdogan amesema ni lazima nchi zote zipaze sauti zao dhidi ya mzozo wa kibinadamu katika eneo hilo.

Türkei Erdogan Rede Parlament
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: AFP

Hapo jana Erdogan alitangaza kuwa amefuta ziara aliokuwa amepanga kufanya nchini Israel kutokana na kile alichokiita "vita vya kinyama" dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza. Rais huyo wa Uturuki ameongeza kuwa haizingatii Hamas kama kundi la kigaidi bali kama "wakombozi" wanaopigania ardhi yao, na ambao wanalaaniwa kutokana na hasira ya serikali ya Israel.

Vita kati ya Israel na Hamas tayari vimesababisha maafa makubwa kwa pande zote mbili. Wizara ya Afya huko  Gaza  imesema hapo jana kwamba angalau Wapalestina 6,546 wameuawa na wengine 17,439 wamejeruhiwa. Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa na wengine 1,650 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel baada ya shambulio la kushtukiza la Hamas la Oktoba 7 kusini mwa Israel lililosababisha pia vifo vya watu 1,400 huku wengine zaidi ya 200 wakichukuliwa mateka.