1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Migogoro inachangia hali ya njaa duniani

Bruce Amani
31 Januari 2018

Umoja wa Mataifa umesema kuwa migogoro inaendelea kuchangia hali ya njaa duniani na kuifanya kuwa mbaya zaidi, na hivyo umetoa wito wa kufanywa juhudi kubwa za kutafuta amani ili kumaliza baa la njaa

https://p.dw.com/p/2roHM
Uganda Bürgerkrieg und Hunger im Südsudan treiben Menschen zur Flucht
Picha: Getty Images/D. Kitwood

Ripoti ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani – WFP na shirika la Chakula na Kilimo – FAO iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama imesema kuwa katika nchi nane zinazokabiliwa na hali mbaya ya njaa duniani, karibu mtu mmoja kati ya wanne hapati mlo.

Karibu watu milioni 17 ambayo ni asilimia 60 ya idadi ya watu nchini Yemen wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa, ikifuatwa na Sudan Kusini ambapo asilimia 45 ya watu hawana chakula cha kutosha. Hii leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashugulikia Watoto – UNICEF limetoa ombi la dola bilioni 3.6 za kutoa msaada wa kiutu kwa watoto milioni 48 walioathiriwa na machafuko na migogoro ya kivita. Kumaliza njaa na utapia mlo ifikapo mwaka wa 2030 ni moja ya malengo kabambe yaliyowekwa na serikali mbalimbali katika mwaka wa 2015.

Lakini viwango vya njaa vimepanda katika mwaka wa 2016 kwa mara ya kwanza katika Zaidi ya muongo mmoja hadi watu milioni 815, kutoka idadi ya watu milioni 777 katika mwaka wa 2015, wakati kukiwa na mizozo, mabadiliko ya tabia nchi na matatizo ya kiuchumi.

Hungersnot im Jemen, Südsudan und in Somalia
Migogoro inachangia katika hali ya njaa dunianiPicha: obs/UNO-Flüchtlingshilfe/UNHCR/M. Hamoud

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha wengi wa watu wanaokumbwa na njaa ambao ni milioni 489 wanaishi katika nchi ambazo zinakabiliwa na vita. Ripoti hiyo iliangazia nchi 16 duniani, pamoja na kanda ya Mto Chad ya Afrika Magharibi, ambayo inakabiliwa na hatari kubwa ya kuzuka njaa.

Syria na Lebanon – ambayo inawahifadhi mamilioni ya wakimbizi wa Syria, zilichukua nafasi ya tatu kati ya nchi zilizoathirika Zaidi na njaa, huku asilimia 33 ya watu wakikosa chakula.

Nchi mbili, Afghanistan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Nchini Afghanistan, watu milioni 7.6 wanahitaji msaada, huku wengi wakiwa katika maeneo mengi ambayo hayafikiki kwa urahisi na mashirika ya misaada na ambayo pia kuna makundi ya wapiganaji.

Ripoti hiyo imesema hali nchini Congo pia inaendelea kuwa mbaya, ambapo watu milioni 7.7 wanahitaji chakula, ikiwa ni ongezeko la karibu watu milioni 2 tangu mwaka wa 2016. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitambuliwa kuwa mgogoro uliopuuzwa kabisa katika mwaka wa 2017, kwa mujibu wa utafiti wa shirika la Thomson Reuters.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu