1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu milioni 65 walipoteza makaazi 2015

20 Juni 2016

Leo ikiwa ni siku ya Kimataifa ya Wakimbizi, Umoja wa Mataifa umesema watu waliopoteza makaazi ya kote duniani imefikia rekodi mpya. Ujerumani iliyapokea maombi mengi ya hifadhi kuliko nchi nyingine yoyote

https://p.dw.com/p/1J9q5
Griechenland Flüchtlingscamp in Idomeni
Picha: Diego Cupolo/DW

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi – UNHCR limesema kuwa kiwango cha mateso na mizozo katika nchi kama vile Syria na Afghanistan kimeongeza idadi ya wakimbizi na watu walioachwa bila makao nchini mwao kote duniani kufikia watu milioni 65.3 hadi mwishoni mwa mwaka jana, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Mwaka uliotangulia, wa 2014, ulikuwa tayari umeshuhudia idadi kubwa ya wakimbizi kote duniani tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo watu milioni 60 waliachwa bila makaazi. Lakini mwaka jana – wakati Ulaya iliyumba kutokana na mmiminiko wa wahamiaji – uliongeza idadi hiyo kwa karibu asilimia 10 kwa mujibu wa takwimu za UNHCR.

Afrika Kenia UN Abgeordneter für Flüchtling Filippo Grandi
Filippo Grandi, Kamishena wa Umoja wa Mataifa kuhusu WakimbiziPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Senosi

Shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva limewaomba viongozi wa UIaya na kwingineko kuchukua hatua zaidi ili kumaliza vita ambavyo vinasababisha mmiminiko wa watu kutoka manyumbani mwao. Filippo Grandi ni kamishena mkuu wa Umoja wa Mataifa "Kile wakimbizi na wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterania na kuwasili katika fukwe za Ulaya, ujumbe ambao wanaubeba ni kuwa iwapo hautayatatua matatizo, matatizo yatakukujia. Na huo ni ujumbe mkali".

UNHCR inasema kuwa kwa kiwango cha wastani, watu 24 walipoteza makaazi kila dakika, kila siku mwaka jana – au watu 34,000 kwa siku – ikiwa ni kutoka idadi ya watu sita kila dakika katika mwaka wa 2005. Idadi ya watu waliopoteza makaazi kote duniani imeongezeka maradufu tangu mwaka wa 1997, na kuongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka wa 2011 pekee – wakati vita vya Syria vilianza.

Zaidi ya nusu ya wakimbizi wote walitokea nchi tatu: Syria, Afghanistan na Somalia. Uturuki ndiyo nchi iliyoongoza kwa kutoa hifadhi kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kuwapa hifadhi karibu watu milioni 2.5 – karibu wote kutoka nchi jirani Syria. Nchi jirani ya Afghanistan, Pakistan ilikuwa na watu milioni 1.6, wakati Lebanon, Syria, iliwapa hifadhi watu milioni 1.1.

wakimbizi wa Kirundi nchini Tanzania
wakimbizi wa Kirundi nchini TanzaniaPicha: Reuters/T. Mukoya

Watunga sera na makundi ya uhamasishaji yanakiri kukabiliana na changamoto kubwa za kuwasaidia watu wengi walioachwa bila makaazi: ambao ni karibu watu milioni 40.8 wanaoishi katika kambi za ndani mwa nchi zenye migogoro.

Grandi amesema zaidi ya watu milioni moja walikimbilia Ulaya mwaka jana, na kusababisha mzozo wa kisiasa katika Umoja wa Ulaya. "Hakuna mpango mbadala kwa Ulaya katika siku zijazo, hakuna mpango mbadala. Ulaya, imekuwa, na itaendelea kuwapokea waomba hifadhi. Takwimu huenda zikatofautiana. Natumai zitapungua, maana kuwa matatizo yatapungua. Kwamba labda kutakuwa na msaada zaidi kwa nchi nyingine kuwapa hifadhi watu hao, lakini haliepukiki".

UNHCR imezitolea wito nchi kupambana na chuki dhidi ya wageni ambayo imeandamana na ongezeko la idadi ya wakimbizi, na ukalalamikia vizuizi vinavyowekwa kama vile nyua zinazojengwa na baadhi ya nchi za Ulaya – pamoja na vya kisheria ambavyo vinawazuia wakimbizi kuingia katika nchi tajiri na zenye utulivu zaidi.

Takwimu zinazozusha hofu katika ripoti hiyo zinaonyesha kuwa watoto walijumuisha asilimia 51 ya idadi ya wakimbizi kote ulimwenguni mwaka jana. Wengi watoto hao walipoteleana na wazazi wao au walisafiri peke yao, ambapo zaidi ya maombi ya hifadhi 98,400 yaliwasilishwa na watoto ambao hawakuandamana na wazazi.

Shirika la kuwashughulikia watoto nchini Ujerumani limetoa wito wa kupewa elimu watoto wakimbizi zaidi ya 8,500 ambao wazazi wao hawajulikani waliko. Mkuu wa shirika hilo Thomas Kruger ameliambia gazeti la “Neue Osnabrücker Zeitung” kuwa watoto hao wanakabiliwa na kitisho cha kuingia katika ukahaba, utumwa, au hata kuuzwa kwa ajili ya biashara haramu ya viungo vya mwili.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo