1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaipa mamlaka zaidi tume ya Sudan Kusini

Grace Kabogo
24 Machi 2017

Tume ya Umoja wa Mataifa inayochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu Sudan Kusini, sasa imepewa mamlaka zaidi ya kuchunguza ukiukaji wa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/2ZuYy
Antonio Guterres
Picha: picture-alliance/dpa/J.-Ch. Bott

Tume hiyo itachunguza vitendo vya ukiukaji kama vile ubakaji wa watu wengi na mateso ambavyo vimefanywa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu nchini humo kwa muda wa miaka mitatu.

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, leo limeipatia tume hiyo mamlaka ya kukusanya na kuhifadhi ushahidi na kuwataja watu wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo.

Mraghibishi kutoka shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, Laila Matar, amesema katika taarifa yake kwamba baraza hilo limechukua hatua muhimu kuelekea katika uwajibikaji.

Uchunguzi huo wa Umoja wa Mataifa ulianza mwaka mmoja uliopita kuorodhesha vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu nchini Sudan Kusini. Tangu wakti huo, makubaliano tete ya amani yamevunjika na mapigano ya kikabila yamesambaa.

Ukiukwaji unafanywa na vikosi vya usalama vya serikali

Mwezi huu, tume hiyo ya uchunguzi iliripoti kuwa Sudan Kusini ilikuwa inakabiliwa na mauaji ya safisha safisha ya kikabila na hali hiyo inaweza kusababisha mauaji ya kimbari. Kwa mujibu wa tume hiyo, ukiukaji wa haki za binaadamu nchini humo umekuwa ukifanywa na vikosi vya usalama vya serikali.

Südsudan Präsident Salva Kiir und Vizepräsident Riek Machar
Riek Machar (Kushoto) na Rais Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres jana aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba uhalifu wa ukatili umefanyika bila ya woga Sudan Kusini. Ameishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kukataa kuelezea wasiwasi wowote kuhusu kutanuka kwa mzozo huo ambayo sasa unajumuisha baa la njaa.

Matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo yatawasilishwa pia katika mahakama ya Umoja wa Afrika kwa ajili ya Sudan Kusini, ambayo kuanzishwa kwake kumecheleweshwa ingawa jumuiya ya kimataifa imetoa wito kuhusu uwajibikaji wake.

Mzozo wa Sudan Kusini umesababisha moja ya mizozo mikubwa ya kibinaadamu duniani, pamoja na zaidi ya wakimbizi milioni 1.6. Baa la njaa pia limetangazwa katika majimbo mawili ya nchi hiyo, huku zaidi ya watu 100,000 wakiwa wanateseka.

Maelfu ya watu wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilianza Disemba, 2013 kati ya vikosi vinavyomtii Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Afrika Kusini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga