1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yalaani ukandamizaji dhidi ya waandamanaji Kongo

Grace Kabogo
10 Januari 2018

Umoja wa Mataifa umevikosoa vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa ukandamizaji wa kikatili walioufanya dhidi ya waandamanaji na umeitaka mamlaka kuwashtaki wale wote waliohusika na vitendo hivyo.

https://p.dw.com/p/2qbym
Jean-Pierre Lacroix, Blauhelme
Mkuu wa shughuli za kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre LacroixPicha: picture-alliance/AP/Keystone/M. Trezzini

Mkuu wa shughuli za kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix jana ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mzozo kuhusu uhalali wa taasisi za Kongo na kushindwa katika kutekeleza makubaliano ya uchaguzi yaliyofikiwa mwaka 2016, kunachochea watu kukosa subira na kuzuka kwa mivutano iliyosababisha ghasia siku moja kabla ya mwaka mpya.

Lacroix amesema analaani vikali ukandamizaji uliofanywa na vikosi vya usalama vya serikali dhidi ya maandamano yaliyoandaliwa na vyama vya kiraia Disemba 31. Ameongeza kusema kuwa viongozi lazima wafanye uchunguzi kuwabaini waliohusika na ukiukaji wa haki za binaadamu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kiasi ya watu watano waliuawa wakati wa maandamano hayo, baada ya polisi kuvamia makanisa, kutumia mabomu ya kutoa machozi na kufyatua risasi hewani wakati wakiwatawanya waandamanaji kwenye mji mkuu wa Kongo, Kinshasa na katika mji wa Kananga. Zaidi ya makanisa 160 yalishiriki katika maandamano hayo.

Unruhen im Kongo
Waandamanaji wa KongoPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Maandamano hayo yalifanyika wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu yalipofikiwa makubaliano ya kisiasa yaliyokuwa yakisimamiwa na Kanisa Katoliki ambayo yangefungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi mwaka 2017 na kumalizika kwa utawala wa Rais Joseph Kabila. Hata hivyo, uchaguzi huo ulisogezwa mbele hadi Disemba, 2018.

Wahusika wa kisiasa wajizuie na ghasia

Lacroix amezitaka sekta zote zinazohusika katika siasa za Kongo kujizuia na vitendo vya ghasia na kwamba mazungumzo ndiyo njia pekee itakayoituliza hali ya kisiasa nchini humo.

''Ni muhimu kwa watendaji wote wa kisiasa kuhakikisha wanaizingatia tarehe ya uchaguzi. Serikali, vyama vinavyoiunga mkono serikali, upinzani na vyama vya kiraia pamoja na tume ya uchaguzi, wote wanapaswa kutoa mchango wao katika kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi yanaendelea kwa wakati,'' alisema Lacroix.

Rais Kabila aliyechukua madaraka mwaka 2001, alikataa kuachia madaraka baada ya kipindi chake cha pili kukamilika Disemba, 2016. Balozi wa Kongo katika Umoja wa Mataifa, Ignace Gata Mavita, ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba serikali yake imesikitishwa na ghasia hizo, na kwamba maafisa watachunguza vitendo vilivyofanywa na vikosi vya usalama, baada ya kuvamia makanisa.

Joseph Kabila Präsident der Demokratischen Republik Kongo
Rais wa Kongo, Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Hata hivyo, balozi huyo ameushutumu upinzani kwa kujaribu kudhoofisha mchakato wa uchaguzi kwa kufanya maandamano. Ufaransa imetoa wito wa kufikishwa katika vyombo vya sheria wale wote waliohusika na vitendo hivyo. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, amesema Rais Kabila anapaswa kuviwajibisha vikosi vyake vya usalama, kuheshimu haki za binaadamu za raia wake na kuachia madaraka, kufuatia uchaguzi wa Disemba.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa linakutana kwa mara ya kwanza kuijadili hali ya kisiasa nchini Kongo, tangu tarehe 23 Disemba, 2018 ilipotangazwa kuwa siku ya uchaguzi wa kihistoria nchini humo. Baraza hilo linaunga mkono tarehe mpya ya uchaguzi na limeonya pasiwepo na ucheleweshwaji mwingine wowote.

Wakati huo huo, awamu ya kwanza ya mashine nane za kupigia kura imeanza kuwasili Kongo kutoka Korea Kusini. Tume ya Uchaguzi CENI, imesema mashine hizo zimewasili jana kwa lengo la kutoa elimu ya uraia na uchaguzi kwa Wakongo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga