1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

UN yaomba ufadhili zaidi wa wakimbizi wa Sudan

Lilian Mtono
1 Februari 2024

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu walioyakimbia makazi yao kutokana na vita kati nchini Sudan imekaribia milioni nane na kutoa rai kwa wahisani kuongeza ufadhili ili kukabiliana na janga hilo.

https://p.dw.com/p/4buiS
Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa Filippo Grandi
Mkuu wa Shirika la kuhudumia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi ameonya juu ya janga kubwa la kibinaadamu nchini Sudan kutokana na ongezeko la wakimbiziPicha: Sakchai Lalit/AP Photo/picture alliance

Umoja wa Mataifa umeliita janga hilo la wakimbizi wa Sudan kuwa ni la "kutisha."

Umoja wa Mataifa unatoa takwimu hizi wakati kukiwa na taarifa kwamba maafisa wa ngazi za juu wa pande zinazohasimiana nchini humo wamekutana mara tatu mwezi Januari huko Bahrain. 

Kamishna wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Filippo Grandi anayezuru nchini Ethiopia amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa kwamba mzozo umezidi kuongezeka na raia wanazidi kuathirika.

Amesema ni karibu mwaka mmoja sasa, watu milioni nane wameyakimbia makazi yao nchini Sudan na kuongeza kuwa zaidi ya wengine milioni 1.5 wamekimbilia kwenye mataifa sita yanayopakana na Sudan.

Soma zaidi: Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa laezea kushtushwa na kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan

Grandi, ambaye alizuru pia taifa la Sudan akatoa mwito kwa wafadhili kuongeza msaada kwa ajili ya wakimbizi hao, kwa kuwa ni asilimia 40 tu ya ufadhili ambayo imetolewa hadi sasa na kuonya kwamba hilo halikubaliki, kwa kuzingatia baadhi ya mizozo hivi sasa ndio inatupiwa macho zaidi.

"Halafu nchi za Ulaya zinalalamika kwamba watu wanakimbilia kwao kupitia Mediterania, Libya, Tunisia... unajua yote haya. Kwa kweli, nina ujumbe. Nina ujumbe kwa nchi hizi zote, ikiwa hatutawekeza zaidi, wala kutawatuliza watu hawa....na msaada wa kibinaadamu ni hatua ya kwanza ya kuwatuliza ili wasiondoke," alisema Grandi.

Mvutano kati ya jeshi la Sudan na RSF

Maandamano ya kukipinga kikosi cha RSF huko Wad Madani nchini Sudan
Watu wanaounga mkono jeshi la Sudan wakiandamana katika mji wa Wad Madani Disemba 17, 2023 katikati ya vita dhidi ya RSFPicha: AFP

Mvutano baina ya mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na aliyewahi kuwa naibu wake Mohamed Hamdan Daglo  anayeongoza kikosi cha wanamgambo wa RSF ulianza mwezi Aprili mwaka uliopita.

Juhudi za kidiplomasia za kumaliza mapigano hayo zimeendelea na hata baada ya makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano kukiukwa.

Lakini taarifa zilizotolewa jana Jumanne zimesema maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Sudan, SAF na RSF wamekutana mara tatu katika kipindi cha mwezi wa Januari huko Bahrain hii ikiwa ni kulingana na duru zenze uelewa na mikutano hiyo ambayo ni ya kwanza ya aina hiyo kati ya pande hizo zinazohasimiana.

Tofauti na mazungumzo ya awali juu ya vita hivyo, mikutano hii ya Manama ilihudhuriwa na mawaziri wenye ushawishi mkubwa kutoka pande zote mbili na maafisa kutoka Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa majeshi yote mawili, vimesema vyanzo vinne, ambapo viwili kati yao vilihudhuria mazungumzo.

Soma zaidi: Mazungumzo ya kutafuta amani ya Sudan yakwama Jeddah

Lakini kwa uchache vilisema mwakilishi wa jeshi na mwenye misimamo mikali Jenerali Shamseldin Kabbashi na Jenerali Abdelrahim Daglo wa RSF ambaye ni kaka wa kamanda Hamdan Daglo, walihudhuria.

Mazungumzo hayo ambayo hayakutangazwa, ambayo kulingana na vyanzo hivyo pia yalihudhuriwa na Marekani na Saudi Arabia yanafanyika baada ya majaribio kadhaa yaliyoshindwa yaliyoongozwa na mataifa hayo makubwa pamoja na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuratibu makubaliano ya kisiasa na usitishwaji wa mapigano ili hatimaye kuvimaliza vita hivyo.

Majadiliano zaidi yameandaliwa juu ya hatua za kusitisha mapigano lakini mkutano uliopangwa wiki iliyopita uliahirishwa.