1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka uchunguzi kuhusu kifo cha mwanaharakati wa Libya

Lilian Mtono
22 Aprili 2024

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoisaidia Libya umetoa wito jana Jumapili wa uchunguzi wa kifo cha mwanaharakati wa kisiasa aliyekuwa akizuiwa katika kambi moja kijeshi mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4f2cS
Khalifa Haftar-Libya
Mbabe wa kivita wa Libya, Khalifa KhaftarPicha: Abdullah Doma/AFP

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoisaidia Libya umetoa wito jana Jumapili wa uchunguzi wa kifo cha mwanaharakati wa kisiasa aliyekuwa akizuiwa katika kambi moja kijeshi mashariki mwa nchi hiyo inayodhibitiwa na mbabe wa kivita, Khalifa Khaftar.

Ujumbe huo aidha ulitaka kuachiliwa huru mara moja kwa wafungwa wengine, ambao amesema walikuwa wanashikiliwa na mamlaka za eneo hilo kinyume na sheria.

Soma: Makazi ya waziri mkuu wa Libya yashambuliwa

Kwenye taarifa yake katika mtandao wa X, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umesema umesikitishwa sana na kifo cha mwanaharakati huyo Siraj Dughman na kuzionya mamlaka za eneo hilo la mashariki kufanya uchunguzi wa uwazi na huru juu ya kisa hicho.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, Dughman alikamatwa kinyume cha sheria na kufungwa mwaka 2023, pamoja na watumishi wengine wa taasisi yake ya Center for Future Studies walioko Benghazi, bila ya kushitakiwa ama kufikishwa mahakamani.