1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatakiwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya Libya

26 Februari 2011

Balozi wa Libya kwenye Umoja wa Mataifa, Mohammed Shalgham, amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kuwalazimisha viongozi wa Libya kuacha kutumia nguvu nchini humo.

https://p.dw.com/p/10Pp3
Balozi wa Libya kwenye Umoja wa Mataifa, Mohamed ShalghamPicha: AP

Akizungumza na waandishi habari baada ya kikao maalum cha Baraza la Usalama, Bwana Shalgham alisema nguvu inayotumika nchini Libya dhidi ya raia lazima ikomeshwe.

Hata hivyo, mwanadiplomasia huyo alikuwa wazi kwamba hatua zozote zinazotakiwa kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa zitakuwa vikwazo dhidi ya kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi na familia yake na sio dhidi ya watu wa Libya.

Kwa upande mwingine mataifa ya Umoja wa Ulaya yamekubaliana kimsingi kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya Libya, pamoja na kuzuia viza na mali za viongozi wa utawala wa Muammar Gaddafi. Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ujerumani, imesema kuwa vikwazo hivyo vitahusu vifaa vya kijeshi na mali ambazo zinaweza kutumika kuwakandamiza waandamanaji wanaopigania demokrasia.

EU Gipfel in Brüssel Merkel Sarkozy Barroso
Baadhi ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa UlayaPicha: AP

Vikwazo hivyo vinatarajiwa kuanza kutumika wiki ijayo. Duru za kidiplomasia zimeeleza kuwa mataifa ya kusini mwa Umoja wa Ulaya kama vile Italia, yamekuwa yakisita kuweka vikwazo zaidi kwa hofu kwamba Gaddafi anaweza kulipiza kisasa dhidi ya maelfu ya raia wa umoja huo ambao bado wako nchini Libya.

Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani, pia ametangaza kuandaa vikwazo vinavyomlenga Gaddafi. Rais Obama ametia saini amri maalum ya kuzuia mali zinazomhusu Gaddafi na familia yake, akiongeza kuwa vikwazo hivyo havilengi mali za watu wa Libya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPA,AFP,AP,RTRE)
Mhariri: Sekione Kitojo