1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNCTAD: Changamoto na nafasi zinazotokana na utandawazi

18 Aprili 2008

Binadamu wote tunaishi katika sayari moja,lakini tunaishi kati hali zinazotofautiana sana.Ukweli huo hasa umedhihirika kufuatia mzozo wa hivi sasa wa kuongezeka kwa bei za vyakula.

https://p.dw.com/p/Dk9K

Tofauti hizo zikitiwa maanani,mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) katika mji mkuu wa Ghana,Accra unatafuta njia ya kupata usawa katika enzi hii ya utandawazi.

Mkutano wa UNCTAD kuanzia tarehe 20 hadi 25 Machi utachunguza nafasi na changamoto zinazotokana na utandawazi.Mada zitakazojadiliwa zinahusika na mzozo wa sasa wa kuongezeka kwa bei za vyakula,hadi kuporomoka kwa hisa katika masoko ya fedha duniani pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.Kwani masuala hayo yote yanahusika na ulimwengu unaozidi kuwa kama kijiji katika enzi hii ya utandawazi.

Lakini mkutanoni Accra,haitazamiwi kuwa kutatiwa saini mikataba fulani au maamuzi ya mwisho yatapitishwa. Ingawa ni mkutano mmojawapo unaofanywa kila baada ya miaka minne,safari hii una muhimu mkubwa.Kwa maoni ya Detlef Kotte alie Mkuu wa idara inayoshughulikia mikakati ya uchumi na siasa za maendeleo katika shirika la UNCTAD,mkutano wa safari hii unafanywa wakati muafaka.Anasema,kwenye mkutano wa Accra,matokeo ya utandawazi na hata mfumo wa sheria za kimataifa kuhusika na siasa za uchumi ni sehemu muhimu ya mada za mustakabali wa dunia nzima.Ni dhahiri kuwa utandawazi ndio uliozusha mzozo wa vyakula unaoshuhudiwa hivi sasa kote duniani.Detlef Kotte akaongezea:

"Bila shaka,suala la kupambana na mzozo uliopo hivi sasa, litachukua nafasi muhimu katika midahalo mingi.Kwa mfano, kikao kimoja kitashughulikia utandawazi na jinsi unavyoathiri jamii na umasikini.Mzozo wa chakula, umedhihirisha kuwa hakuna nchi inayowezayo kujitenzulia tatizo hilo peke yake.Ni tatizo la dunia nzima na limekuwa sehemu ya utandawazi na juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa."

Wataalamu wote wanakubaliana kuwa hatua za kuhimiza kote duniani kuzalisha mafuta kutokana na mimea, ndio kumesababisha kuongezeka kwa bei za vyakula kila pembe ya dunia.Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO,katika mwaka 2007 peke yake vyakula vimeongezeka bei kwa takriban asilimia 40. Isitoshe,katika nchi kama China na India kuna mahitaji makubwa ya nyama na maziwa-matokeo yake ni kuongezeka kwa bei za nafaka kama vile ngano,mahindi na maharage ya soya-chakula kinachohitajiwa kwa wingi kuwalisha wanyama.Kwa upande mmoja,kuongeza kula nyama ni ishara ya hali bora ya maisha lakini masikini wanaathirka vibaya mno.

Mkutano wa UNCTAD mjini Accra ndio utajaribu kutafuta njia ya kuwa na ugavi wa haki.