1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR kumaliza tatizo la wasio na Uraia

4 Novemba 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi-UNHCR limeanzisha kampeni inayolenga kumaliza tatizo la watu wasio na uraia, ambao kwa mujibu wa shirika hilo wanafikia milioni 10 kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/1DgQn
Mkutano wa UNHCR ulioanzisha kampeni dhidi ya hali ya kutokuwa na uraia
Mkutano wa UNHCR ulioanzisha kampeni dhidi ya hali ya kutokuwa na uraiaPicha: picture-alliance/dpa/S. Di Nolfi

Kampeni hiyo imeanzishwa chini ya kaulimbiu ijulikanayo kwa lugha ya kiingereza kama ''I belong''. Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi-UNHCR limesema kupitia kampeni hiyo linataka kuzimulika changamoto wanazokabiliana nazo watu wasio na uraia, na kuzihimiza nchi kuzirekebisha sheria zao ili asiwepo mtu anayejikuta katika hali ya kutokuwa raia wa nchi yoyote.

Mkurugenzi wa UNHCR Antonia Guterres amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, kwamba kila dakika 10 anazaliwa mtu asiyekuwa na uraia wa taifa lolote ulimwenguni, na kwamba kutokuwa na uraia huwafanya watu hao kuhisi kama kuwepo kwao ni makosa. Guterres ameongeza kuwa hilo halikubaliki katika karne ya 21.

''Watu wasio na uraia hunyimwa haki zao za kimsingi, kama vile kuandikishwa kisheria wanapozaliwa, kwenda shule, huduma za afya, ndoa na nafasi za ajira, na hata kunyimwa hati ya kifo pale wanapoiaga dunia'', imesema ripoti ya shirika hilo.

Ukosefu wa uraia hutokana na sababu nyingi

Watu wanaweza kunyimwa uraia kutokana na sababu mbali mbali, zikiwemo za ubaguzi wa kikabila, wa kimadhehebu na hata wa kijinsia. Hali hiyo pia yaweza kutokea pale mataifa yanaposambaratishwa na vita au mizozo.

Watu wa jamii ya Rohingya: Myanmar na Bangladesh zimekuwa zikiwatupiana kama mpira
Watu wa jamii ya Rohingya: Myanmar na Bangladesh zimekuwa zikiwatupiana kama mpiraPicha: picture-alliance/dpa

Idadi kubwa ya watu wasio na uraia hupatikana nchini Myanmar, ambako serikali ya nchi hiyo haiwatambui watu wa jamii ya Rohingya ambao ni waislamu. Guterres amesema idadi ya watu hao ni takribani milioni moja.

Myanmar huwachukulia watu hao kuwa wahamiaji kutoka Bangladesh, nchi ambayo pia huwachukulia wale wanaovuka mpaka kutoka Myanmar kuwa wahamiaji haramu.

Kusambaratika kwa mataifa

Idadi nyingine kubwa ya watu wasio na uria wapatao 600,000 ilitokana na kuvunjika kwa Muungano wa Kisovieti wa Urusi miaka zaidi ya 20 iliyopita.

Changamoto za kukosa uria pia huwakumba watu waliozikimbia nchi zao. Kwa mfano, asilimia 70 ya watoto wanaozaliwa na wakimbizi kutoka Syria walioko Lebanon na Jordan hawapati vyeti vya kuzaliwa, amesema Antonio Guterres.

Katika nchi kama Iran na Qatar, wanawake hawana haki ya kuwarithisha watoto uraia wao kama ilivyo kwa wanaume, na katika mazingira hayo wanaweza wakawepo maelfu ya watu wasio na uraia kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Askofu Desmond Tutu, mmoja wa watu wanaofanya kampeni kumaliza tatizo la watu wasio na uraia
Askofu Desmond Tutu, mmoja wa watu wanaofanya kampeni kumaliza tatizo la watu wasio na uraiaPicha: picture-alliance/dpa

Idadi ya watu milioni 10 wasio na uraia haiwajumuishi wapalestina, kutokana na kwamba taifa lao limetambuliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Kampeni hii ya UNHCR inaungwa mkono na Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, na mcheza filamu maarufu Angelina Jolie kutoka Marekani. Inalo lengo la kukusanya sahihi milioni 10, kwenye hati inayotaka kumalizika kwa tatizo la kutokuwa na utaifa.

Habari njema ni kwamba katika muongo mmoja uliopita watu zaidi ya milioni nne ambao awali hawakuwa na utaifa wamefanikiwa kuupata, kutokana na mabadiliko ya sera katika baadhi ya mataifa. Katika hatua kama hiyo, Bangladesh ilipitisha sheria mwaka 2008, ambayo iliwapa watu 300,000 wanaozungumza lugha ya Urdu uraia wa nchi hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ AFPE/RTRE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir