1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF kupambana na ukatili dhidi ya watoto walemavu

31 Mei 2013

Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, limeripoti watoto wenye ulemavu ulimwenguni ni waathiriwa wakubwa wa mateso, ubakaji na wengi wao hawasajiliwi baada ya kuzaliwa ikilinganishwa na wasiokuwa na ulemavu.

https://p.dw.com/p/18hc1
Mdau wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu watoto UNICEF
Mdau wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu watoto UNICEFPicha: dapd

Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF iliyotolewa jana katika mkutano wake mjini Da Nang, Vietnam, watoto wenye ulemavu wanabaguliwa na kutengwa katika jamii kwa sababu wazazi hawatoi uangalizi wa kutosha kwa watoto hao, likiwemo la kutowaandikisha wanapozaliwa.

Mkugenzi Mkuu wa UNICEF, Anthony Lake, amesema ukosefu wa takwimu za watoto walemavu katika nchi nyingi duniani, umewafanya watoto hao kutokujuilikana na kutambuliwa. UNICEF inakadiria kuwa kila penye watoto 20 wenye umri wa miaka 14, mmoja wao ni mlemavu wa moja kwa moja au anaishi na aina fulani ya ulemavu.

Lake amesema hali inayowakabili watoto wenye ulemavu duniani ni ya kutisha, na kutowasajili kumechangia sana mateso na idhilali juu yao, huku wengi wao wakikosa msukumo wowote wa kuwaendeleza kama watoto.

Haja ya kujua  idadi ya walemavu duniani ni muhimu

Mkurugenzi huyo ameongeza kusema na hapa namnukuu: "Kama hatutakuwa na mfumo wa kujua idadi ya watoto wenye ulemavu, hatutaona umuhimu wao."

Kijana mwenye ulemavu wa miguu
Kijana mwenye ulemavu wa miguuPicha: picture-alliance/dpa

Miongoni mwa unyanyasaji unaowakabili watoto hao ni ule unaohusiana na ngono. Kutokupewa elimu ya mahusiano na madhara ya magonjwa ya zinaa kunawaweka watoto hao katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa hayo.

Kwa kukosa kwao mafungamano ya kawaida ya kibinaadamu, watoto wengi wenye ulemavu wanakuwa wakimya na wanashindwa kujua mipaka katika mahusiano yao na wengine.

Pamoja na mengine, ripoti hiyo ya UNICEF inagusia vitendo vya kuwawinda na kuwakata viungo watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania kwa imani za kishirikina, ikiitaka jamii kubadili mtazamo wake kuhusu watoto wenye ulemavu, kwa kuwapatia huduma za kijamii, ikiwemo elimu na afya

Ripoti hiyo imetaka msisitizo mkubwa uwekwe katika kile ambacho watoto wenye ulemavu wanaweza kufanya kulikoni kuangalia tu katika kile wasichoweza kufanya watoto hao.

''Mara nyingi nimeona katika televisheni watoto wenye ulemavu hawapati fursa ya kwenda skuli, kutokana na mtazamo wa watu kuhusu watoto walemavu, ambao sio sahihi,'' amesema Nguyen Phoung Anh mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 kutoka Vietnam.

Phoung Anh mwenye maradhi ya mifupa, amekuwa mtu mashuhuri sana nchini Vietnam, baada ya kuonesha kipaji chake katika televisheni ya nchi hiyo akiimba na kucheza akiwa katika kiti chake. Anasema licha ya kila mtu kujua kuwa ni kosa kuwatenga watu wenye ulemavu, bado watu wanawachukulia vibaya watu wenye ulemavu kama vile sio binadamu wa kawaida.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtoto wa kike mwenye ulemavu yuko kwenye hatari kubwa zaidi kuliko mwenzake wa kiume, na amekuwa akiachwa nyuma sana katika kila jambo.

UNICEF imeitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza nguvu zaidi katika kupambana na matatizo yanayowakabili watoto wenye ulemavu, kwani dola milioni 100 zilizotolewa na wafadhili ni  thuluthi moja  tu ya zile zinazojitaka kuwasaidia watoto hao.

Mwandishi: Hashimu Gulana/AFP/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef