1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Union Berlin wapokea kipigo cha 3-0 nyumbani

4 Septemba 2023

Union Berlin imepoteza mechi yake ya kwanza nyumbani, kwa kipigo cha 3-0 dhidi ya RB Leipzig (MD3), tangu Februari 2022, ilipopokea kichapo sawa na hicho kutoka kwa Borussia Dortmund.

https://p.dw.com/p/4VvYn
Fussball Bundesliga - RB Leipzig v Union Berlin
Picha: opokupix/IMAGO

Maji yalizidi unga upande wa Union pale mchezaji Kevin Volland alipoonyeshwa kadi nyekundu, lakini Kocha Urs Fischer alipongeza mapambano ya timu yake na kusema ni vigumu kupata ushindi dhidi ya mpinzani kama Lepizig hasa ukiwa bila ya mchezaji mmoja.

Xavi Simons alipachika wavuni bao la ufunguzi dakika ya 51 ya mchezo huku mchezaji Benjamin Šeško akifunga mabao mawili dakika ya 85 na 87.

Soma pia: Timu zilizopanda daraja Bundesliga ziko hoi

Katika mechi nyengine Niels Nkounkou alifunga bao lake la kwanza zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya mechi kukamilika na kuipa Eintracht Frankfurt pointi moja katika sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya FC Cologne.

Beki huyo wa Ufaransa, ambaye alisajiliwa kutoka Saint Etienne siku ya Ijumaa, aliisawazishia Frankfurt akitokea benchi baada ya Cologne kuongoza mechi hiyo kupitia mkwaju wa penalti kunako kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji Florian Kainz.

Leverkusen kileleni mwa jedwali

Fußball Bundesliga Bayer Leverkusen - Darmstadt 98 | Torjubel Victor Boniface
Bayer Leverkusen wakisherehea bao la Victor BonifacePicha: Bernd Thissen/dpa/picture alliance

Bayer Leverkusen imetulia kileleni mwa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, baada ya kuicharaza timu iliyopanda daraja msimu huu Darmstadt 98 mabao 5-1 Siku ya Jumamosi.

Mshambuliaji Victor Boniface Mnigeria ambaye alijiunga na Leverkusen msimu huu alifunga mara mbili na sasa ana jumla ya mabao manne na amesaidia kuunda mabao 2 katika jumla ya mechi tatu. Mabao mengine ya Leverkusen yalifungwa na Exequiel Palacios, Jonas Hoffman na Adam Hložek. Bao la kufutia machozi la Darmstadt lilitiwa kimyani na Oscar Vilhelmsson.

Baada ya ushindi huu Victor Boniface amesema "Natoa pongezi kwa kocha na wachezaji wote pia kwa jinsi tulivyocheza ni kama tunajuana kwa muda mrefu lakini zaidi na mpongeza kocha kwa sababu anajukumu kubwa kwenye timu."

Granit Xhaka alijivunia matokeo hayo kwa kusema "Huu ni mwanzo tu, tuna timu nzuri, tunaweza kujiimarisha zaidi kama katika kipindi cha kwanza ari zaidi na kudhibiti mpira zaidi lakini kwa ujumla tulicheza vizuri na nina furaha kwamba tumekamilisha mechi 3 kwa jumla ya pointi 9."

Bayern washindwa kukamisha usajili wa kiungo mkabaji

Deutschland Bundesliga Bayern München vs. RB Leipzig | Thomas Tuchel
Kocha wa Bayern Thomas Tuchel Picha: ActionPictures/IMAGO

Na Bayern Munich imeshindwa kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji João Palhinha kutoka Fulham baada ya klabu hiyo kushindwa kupata mchezaji mwengine atakayejaza nafasi yake.  Kuondoka kwa wachezaji kadhaa - kati yao beki Benjamin Pavard, kipa Yann Sommer na winga Sadio Mane, Bayern sasa wana kikosi cha wachezaji 22 na kocha Thomas Tuchel ana wasiwasi katika hatma ya kutetea ubingwa.

Soma pia: Tuchel ataka kukamilisha kileleni mwa Bundesliga

Baada ya tukio hilo rais wa Klabu ya Bayern Munich Uli Hoeness amesema ana matumaini kwamba klabu hiyo itajitahidi kukamilisha usajili wa wachezaji ili kuepueka changamoto za kushindwa kukamilisha usajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho.