1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uongozi mzuri na sera za misaada ya maendeleo

23 Septemba 2009

Ethiopia ni mpokeaji mkubwa kabisa wa misaada ya maendeleo kote duniani,licha ya nchi hiyo kuwa mojawapo ya nchi zenye sifa mbaya katika suala la uongozi mzuri na demokrasia.

https://p.dw.com/p/Jn2S
Bundesentwicklungshilfeministerin Heidemarie Wieczorek-Zeul (SPD) spricht am Donnerstag (16.10.2008) im Bundestag in Berlin im Rahmen der Debatte über eine Verlängerung des ISAF-Mandats für den Bundeswehreinsatz in Afghanistan. Foto: Tim Brakemeier dpa/lbn +++(c) dpa - Report+++
Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani, Heidemarie Wieczorek-Zeul.Picha: picture-alliance/ dpa

Ethiopia ilipoteza sifa yake kufuatia uchaguzi wa mwaka 2005 ulioshuhudia udanganyifu na matumizi ya nguvu. Hata hivyo misaada ya pesa inaendelea kumiminika nchini humo. Kwa mfano, katika mwaka 2007 pekee nchi hiyo ilipokea msaada wa kama dola bilioni mbili. Sasa, wakosoaji ndio wanataka kuona msimamo mkali zaidi ukichukuliwa dhidi ya serikali ya Addis Ababa na hasa kutoka serikali ya Ujerumani iliyo mfadhili mmojawapo mkubwa kabisa wa Ethiopia.Msemaji wa Halmashauri ya haki za binadamu ya Ethiopia nchini Ujerumani, Seyoum Habtemariam anasema:

" Maafisa wahusika wanaifahamu hali inayokutikana nchini Ethiopia.Wao wanajua kuhusu mauaji ya halaiki na ukandamizaji wa kisiasa. Wanaelewa hayo yote lakini hakuna wanachokifanya, badala yake wanashirikiana na serikali ya Ethiopia. Hiyo tutalaani hadharani."

Si wadadisi wote wa Ethiopia waliohamakishwa kama Habtemariam kuhusu sera za serikali ya Ujerumani. Yeye amekwenda umbali wa kulalamika katika ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani katika mahakama ya Karlsruhe dhidi ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri wa Mambo ya Nje Frank-Walter Steinmeier kwa dhana za kwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Hoja ya mashtaka hayo ni kwamba Ujerumani, kwa kutoa misaada ya maendeleo inawezesha ukiukaji wa haki za binadamu nchini Ethiopia.Nchini humo kuna sheria kali zinazoweka vikwazo kwa mashirika yasio ya kiserikali katika sekta ya haki za binadamu na harakati za kuendeleza demokrasia. Kwa mfano, sheria inayoadhibu vikali waandishi wa habari wanaoikosoa serikali, sheria ya kupambana na ugaidi inayovipa vikosi vya usalama uhuru mkubwa wa kupambana na umma na upinzani. Vile vile kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani hivi karibuni Birtukan Medekesa na operesheni ya majeshi ya serikali katika eneo la mvutano la Ogaden.

Orodha ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyotajwa na makundi yanayopigania haki za binadamu nchini Ethiopia ni ndefu mno. Hayo yote yanaambatana vipi na mwongozo wa sera za misaada ya maendeleo na ushirikiano pamoja na nchi zinazofadhiliwa? Mkataba wa serikali ya muungano wa Novemba mwaka 2005 unasema,uongozi mzuri na demokrasia ndilo sharti la kupatikana maendeleo ya maana.

Mwandishi:L.Schadomsky/ZPR/P.Martin

Mhariri: M.Abdul-Rahman